Kanusho hilo limetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa Wizara ya Elimu Oliva Kato, na kueleza kuwa waraka huo batili wa Profesa Bisanda ulitolewa Februari 8, 2021 umeenda kinyume na maelekezo ya Wizara ya Afya na kwamba Wizara inawaelekeza wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho kuendelea na masomo na kazi zao kama kawaida.
Mbali na agizo hilo Wizara ya Elimu pia inatoa rai kwa taasisi zote za elimu nchini kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona na kutoa onyo kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu kuacha kutumia nembo za serikali wanapotoa maoni yao binafsi.
Kwa miezi kadhaa sasa serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuwa hakuna ugonjwa wa Covid-19 - na hivyo hakuna mipango yoyote ya kuwachanja wananchi wake.
Toka mwezi Juni mwaka jana ambapo rais John Magufuli alipotangaza Tanzania haina tena corona, yeye pamoja na viongozi wengine wamekuwa mstari wa mbele kukosoa baadhi ya njia za kupambana na corona na kusisitiza kuwa Tanzania haitatumia mbinu hizo.
Rais Magufuli pia ameonya - bila kutoa ushahidi - kuwa chanjo za Covid-19 zinaweza kuwa na madhara na badala yake amewarai Watanzania kujifukiza na kutumia dawa za asili, ambazo hakuna hata moja iliyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama tiba dhidi ya virusi vya corona.
Ni vigumu kujua kwa nini rais Magufuli amechukua msimamo huo dhidi ya chanjo lakini pia amesema Watanzania wasitumike kama sehemu ya majaribio.
"Kama wazungu wangekuwa na kinga, basi kusingekuwa na Ukimwi, kansa na Kifua Kikuu kufikia sasa," ameeleza Magufuli ambaye amejipambanua kama mtu anayepingana na ubeberu.