Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:36 am

WAZIRI MKUMBO: USIMWITE MWENYE FEDHA FISADI

Waziri wa Uwekezaji nchini Tanzania Prof.Kitila Mkumbo amesema malalamiko makubwa anayoyapokea kutoka kwa wawekezaji walio wengi ni tabia ya watumishi wa Serekali kuwazungusha zungusha wawekezaji hao wanapotaka kuanza kuwekeza mara baada ya Wizara kuwahamasisha juu ya fursa zilizopo nchini.

Kauli hiyo ya Waziri Mkumbo ameitoa hii leo Feb 23, 2021 wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa muongozo wa uwekezaji mkoa wa Singida akiwa ana muwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Dkt Mkumbo amesema tangu ateuliwe kwenye nafasi hiyo, hiyo ndiyo imekuwa changamoto ambayo amekuwa akielezwa kutoka kwa wawekezaji.

“Hatua ya tatu, kuwawezesha wawekezaji na wakati mwingine hapo ndipo tunapofeli mnapiga kelele, mnapiga debe, mnahamasisha wanakuja, wakishakuja hapa tunaanza kuzungushana nenda ofisi ile, lipia kile anazungushwa miezi miwili mitatu , sita au miaka” amesema Prof.Kitila Mkumbo

Aidha amewataka kutengeneza mahusiano baina ya uwekezaji yawe ya kuaminiana na kuacha roho za kizamani na kutowanyooshea vidole wawekezaji pale wanapoanza kupata faida.

“Mahusiano yetu na wawekezaji lazima tuaminiane na tuheshiamiane huwezi kuwa unamuita mwekezaji hapa kesho amewekeza, kijana wa watu amepata pesa mambo yake yamenoga unamuita fisadi unaanza kukasirika we hela umetoa wapi ilihali amefanya biashara, kwahiyo tusichukie watu ambao wana hela na mhe rais amesema watu wenye hela tuwapende kwasababu hakuna aliyekuja kuwekeza ili abaki hivyo alivyo” amesema Prof.Kitila

Aidha Waziri Dkt Mkumbo amewasisitiza wananchi wote wa Singida hususan Mkuu wa Mkoa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji katika zao la alizeti huku akisema kuwa kwasasa kipaumbele kwa alizeti hakiwezi kuwa kiwanda bali uzalishaji.