Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 11:37 pm

UMMY MWALIMU: UGONJWA WA CORONA BADO UPO NCHINI

Serekali ya Tanzania imesema kuwa Ugonjwa wa virusi vya Corona nchini Haujaisha licha ya ripoti ya maambukizi ya ugonjwa huo kupungua nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo June 1, 2020 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, jijini Tanga wakati wa ufunguzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Bodi ya Mkonge Tanzania.

“Tunamshukuru Mungu hali ni nzuri, Tanga hatuna mgonjwa wa corona, kituo kilichokuwa kinatumika kwa wagonjwa wa corona kimefungwa. “Amana tuna wagonjwa watatu, Mloganzila mmoja, Mwanza hakuna mgonjwa. Tunamshukuru Mungu, hata hivyo corona ipo, tuendelee kuchukua tahadhari kujikinga,” amesema Waziri Ummy.

Amesema, Tanzania imefanikiwa katika kudhibiti kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo “corona tumeishinda Tanzania, ukiangalia wenzetu, unajiuliza hivi Tanzania tuna nini? asante Mwenyezi Mungu kwa kutuokoa,” amesema Waziri Ummy

Mara ya kwanza Tanzania iliripoti kisa chake cha kwanza cha ugonjwa wa Covid-19, tarehe 16 Machi 2020, ambapo siku moja baadae ilitangaza kufunga baadhi ya shughuli zenye mikusanyiko ya watu wengi, ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo. Miongoni mwa shughuli zilizofungwa tarehe 17 na 18 Machi 2020 ni, michezo, shule na vyuo vya kati na vikuu, pamoja na shughuli za kijamii. Lakini Mei mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza kufunguliwa kwa vyuo pamoja na shughuli za michezo.