Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:54 am

SPIKA NDUGAI: MBOWE ANAPOTOSHA RIPOTI YA CAG

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amemtuhumu vikali Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA Bw. Freeman Mbowe kwamba anapotosha Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serekali iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Mwezi Marchi 28, 2021 Ikulu ya Dodoma.

Spika amesema Mbowe ambaye alikuwa Mbunge wa Hai ametumwa na Watu wake wa Ulaya kwa lengo la kupotosha mara baada ya Jana Mbowe kusema kuwa alikwenda ulaya kwa lengo la kuwekeza huko na kuchanjwa chanjo ya Corona.

Baada ya Spika Kuona kuwa kunaupotoshaji unaendelea leo amezitaka kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zichambue ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuiwakilisha bungeni haraka katika mkutano wa nne badala ya mkutano wa tano.

Agizo hilo la Spika amelitoa hii leo Jumatatu Aprili 12 2021, Bungeni Dodoma.

Kauli ya Spika Ndugai imekuja siku moja mara baada ya Mwenyekiti huyo wa Chadema kuhutubia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ambapo pamoja na mambo mengine alilituhumu Bunge kwa vitendo vya rushwa na kuchezewa vikali na Muhimili wa Serekali.

“Watu wanabeba tu mabilioni yameibiwa sasa huyo rafiki yangu Freeman Mbowe alikuwa Ulaya huko sasa katumwa na watu wake huko anapotosha mambo,” amesema.

Amesema sio watu wengi wenye uelewa wa kuchambua taarifa za kihasibu na hivyo kunaweza kukawa na ujenzi wa kituo cha afya wa Sh 500milioni lakini Sh 499milioni zimetumika vizuri kabisa.

Spika amesema lakini kati ya fedha hizo Sh1milioni ikikosa kiambatanisho fulani ni kawaida wakaguzi wanahoji fungu zima la Sh 500milioni.

Amesema kwa hiyo unaposoma mtaani unaona sh 500 zimeibwa lakini kumbe pale ni Sh milioni moja ndio hazina risiti.

Amesema kamati hizo zitaanza mapema kuchambua ripoti hizo ili waangalie ratiba yao na kuwaelimisha watu kuhusiana na ripoti ya CAG ambayo ni taarifa nzuri lakini baadhi ya watu wanabeba na kupotosha tu.

Katika Repoti hiyo ya CAG Rais Samia alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari nchini TPA kupisha uchunguzi, kwa sababu ya kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha.