- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
SPIKA MSEKWA: MABADILIKO YA KATIBA MPYA NI JAMBO LISILOEPUKIKA
Ukerewe. Spika wa bunge mstaafu Pius Msekwa amesema kwamba Mabadiliko ya Katiba mpya ni jambo lisilobishaniwa na Haliepukiki kwa sababu mahitaji ya jamii yamebadilika na muda uliopo unasukuma hilo. “Mtu anaweza kuita kivyovyote apendayo; iwe ni Katiba Mpya au mabadiliko ya katiba. Muhimu ni kwamba Taifa letu linahitaji Katiba inayojibu mahitaji kulingana na wakati na mazingira yaliyopo.”
Akihojiwa na gazeti la Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake mtaa wa Kabingo mjini Nansio yaliko Makao Makuu ya Wilaya ya Ukerewe, Mzee Msekwa anasema kinachohitajika katika mchakato huo ni nia njema ya kila mshiriki na wadau wote.
Msekwa ambaye ndiye Makamu Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema umuhimu wa Katiba ni kujibu mahitaji ya jamii, mabadiliko ya nyakati na mazingira yaliyopo ndiyo sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imefanyiwa marekebisho mara 14 hadi sasa.
“Jambo muhimu ni kila mtu anayesukuma na kushiriki mchakato wa kudai mabadiliko ya Katiba kuwa na nia njema ya kudumisha amani, mshikamano, umoja wa kitaifa na undugu miongoni mwa Watanzania.
Kusiwe na mtu anayetaka kuleta vurugu, asiwepo anayetaka kudhulumu haki ya mtu mwingine. Sote tuwe na nia na lengo moja la ustawi, ulinzi na maslahi ya Taifa,” anasema Mzee Msekwa.
Anasema hitaji la jamii na wakati ndivyo husukuma mabadiliko ya Katiba kuruhusu mfumo wa vyama vingi kutokana na vuguvugu lililotokea duniani katika miaka ya 1980.
“Wakati wetu sisi tulianza na mfumo wa chama kimoja katika mazingira yaliyokuwepo ambayo yaliruhusu kuongoza nchi katika mfumo huo. Mambo yalipobadilika katika miaka ya 1980 kutokana na msukumo wa mfumo wa vyama vingi uliosababisha baadhi ya mataifa kuingia kwenye machafuko na kusambaratika kama ilivyotokea kwa Urusi tukalazimika kubadilika,” anasema na kuongeza:
“Tuliona hatuwezi kubaki kama kisiwa katika wimbi hilo la mabadiliko; tukaanza mchakato wa kutafuta maoni ya wananchi kwa Rais wa wakati huo, Ali Hasaan Mwinyi kuunda tume iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ambayo nilipata fursa ya kuwa mjumbe wake”.
Anasema licha ya Watanzania asilimia 80 ya waliohojiwa kuhusu mfumo wa kisiasa kutaka Tanzania iendelee kuwa Taifa la mfumo wa chama kimoja cha siasa huku asilimia 20 pekee wakitaka mfumo wa vyama vingi, wajumbe wa Tume ya Jaji Nyalali na vikao vya CCM akiwemo hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere walishauri kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.
“Tungeweza kutumia usemi wa wahenga wa wengi wape kupendekeza tuendelee kuwa na mfumo wa chama kimoja. Lakini mazingira ya kidunia na mahitaji ya wakati ilitusukuma kupendekeza tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi kwa sababu tusingeweza kubaki kama kisiwa. Tukabadilisha katiba kuruhusu mabadiliko hayo,” anasema
Kwa maoni yake, Mzee Msekwa anaamini msukumo uliokuwepo wakati huo, mahitaji ya jamii na mabadiliko ya nyakati ndio unaosukuma hitaji la kuwa na Katiba inayojibu maeneo yote hayo.
Anatoa mfano wa mfumo wa kisiasa ya uwakilishi Serikali uliopo upande wa Tanzania Bara wa chama kinachoshinda uchaguzi kuchukua vyote kwa kuunda Serikali yenyewe kuwa ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji mabadiliko ambayo lazima yaanzie kwenye Katiba.
“Bunge letu la sasa karibu wabunge wote ni CCM. Zile kura nyingi walizopigiwa wagombea kupitia vyama vya upinzani zimepotea, ni kama hazikuhesabiwa kwa sababu hazina uwakilishi bungeni. Nadhani muda umefika tuwe na mfumo kila kura kuhesabiwa katika uwakilishi bungeni,” anasema Mzee Msekwa, ambaye ni miongoni mwa mwagwiji wa uongozi nchini.
Anasema Taifa linapaswa kuwa na mfumo unaoangalia chama cha pili kwa wingi wa kura kuungana na chama kilichoshinda kuunda Bunge na hatimaye kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Mambo haya yana maelezo mazuri na faida kubwa kwa Taifa, kama tunavyoona hivi sasa upande wa Zanzibar ambako kuna utulivu wa kisiasa kwa sababu kura na maoni ya pande zote za chama tawala na upinzani zinapewa nafasi ya kuingia katika uongozi wa Serikali. Ni jambo zuri sana,” anasisitiza.
Kutokana na umuhimu wa jambo hilo, Mzee Msekwa anasema hata maoni yake mbele ya Kamati ya Rais Samia Suluhu Hassan inayokusanya maoni ya wadau kuhusu masuala ya Katiba na uongozi wa kisiasa yalisisitiza hilo la kuzingatia kura za wagombea wote katika muundo wa Bunge na Seriali.
“Nilishauri ni vizuri tubadilishe mfumo wetu wa uchaguzi kuruhusu vyama vilivyopata kura nyingi kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, siyo Serikali ya mseto. La hasha! Ni Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoshirikisha kura zote walizopata wagombea katika uchaguzi,” anasema.