Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 5:19 pm

NEWS: ZITTO ATAKA UPINZANI KUACHA UBINAFSI

Dar es salaam. Kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo nchini Tanzania Zitto Kabwe, ametoa wito kwa vyama vya upinzani nchini kwamba vinapaswa kuacha ubinafsi kwa kuwa Tanzania ni kubwa kuliko vyama na kwamba Watanzania hawatowasamehe kama hawatoamua kuwa na mgombea mmoja wa Urais, Ubunge na Udiwani.

"Watanzania hawatatusamehe tusipokuwa na mgombea mmoja wa Urais, mgombea mmoja kila Jimbo,na kila Kata, wito wangu kwa viongozi wenzangu wa vyama vya upinzani tuache ubinafsi" amesema Zitto

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 18, 2020, Jijini Dar es Salaam na kusema kuwa mpaka sasa viongozi wanaendelea na mazungumzo kwa ajili ya vyama hivyo kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu ujao na anaamini kuwa Watanzania wengi wanataka mashirikiano.

"Watanzania wanataka ushirikiano ili kuleta mabadiliko katika nchi, na joto la uchaguzi mmeliona watu wamechangamka Bara na Visiwani" amesema Zitto Kabwe.

Zitto ameongeza kuwa yeye na chama chake wako tayari kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuweza kuitoa CCM madarakani.

Zitto amekuwa mwanasiasa wa upinzani nchini anayetaka mshikamano baina ya vyama vya upinzani katika nafasi ya urais.

Kwasasa vyama vyote vikuu vya upinzani nchini vimesimamisha mgombea katika nafasi ya urais kikiwemo chama kikuu cha upinzani cha Chadema ambacho kimemsimamisha Tundu Lissu na ACT Wazalendo yupo aliyekuwa Waziri wa mambo ya njee Bernad Membe.