Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 3:58 pm

NEWS: WATUMISHI 8 WA BENK KUU WABURUZWA MAHAKAMANI

Dar es Salaam. Watu 13 wakiwamo waliokuwa watumishi wanane(8) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamefikishwa katika Mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam wakikabiliwa na mashtaka sita likiwamo la Uhujumu Uchumi, kuharibu noti na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 4.6 bilioni.

Washtakiwa wote hao wamesomewa mashtaka yao hii leo, Desemba 14 na jopo la mawakili 4 wakiongozwa na wakili mkuu wa Serikali, Paul Kadushi akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Godfrey Isaya.

Washtakiwa waliofikishwa Mahakamani ambao ni wafanyakazi wa BOT ni pamoja na Cecilia Mpande (49), Agripina Komba (55), Zubeda Mjewa (50), Khadija Kassunsumo (57) na Mwanaheri Omary (53).

Wengine ni Mariagoreth Kunzugala (29) maarufu kama Bonge, Henry Mbowe (36) maarufu kama Mzee wa Vichwa na Asha Sekiboko (30) wote wanaishi Dar es salaam.

Wengine ambao sio watumishi wa BoT ni Alistides Genand (44) maarufu kama Stide; Musa Chengula(39) maarufu kama Mkinga; Zaituni Chihipo(34) maarufu kama Zai na Respicius Rutabilwa(44) maarufu kama Mtashu.

Akiwasomea hati ya mashtaka, wakili Simon amesema wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 100 ya mwaka 2020 na wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Januari mosi mwaka 2017 na Septemba 30 mwaka 2019 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Katika shtaka la kwanza, kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30 2019, wakiwa Watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Wakili Nyantiro amedai, katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa, katika tarehe hizo na maeneo hayo, jijini Dar es Salaam, washitakiwa Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makusudi, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga.

Katika shitaka la tatu, siku na eneo hilo, washitakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, waliharibu noti 460,000 za Sh 10,000 kila moja kwa kuzikatakata huku zikiwa na thamani ya Sh4.6bilioni

Katika shtaka la nne, siku na maeneo hayo, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washitakiwa wote walijipatia faida ya Sh1.5bilioni kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.

Shitaka la tano ni utakatishaji fedha, ambapo inadaiwa kuwa watumishi hao wa BoT na wenzao ambao sio watumishi, walijihusisha katika miamala tofauti ya Sh1.5 bilioni wakati wakijua zilitokana na kosa tangulizi la uhalifu wa kupangwa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shitaka la sita, washitakiwa wote katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam, waliisababishia BoT hasara ya Sh4.6 bilioni.

Wakili Kadushi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamlika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 28, 2020 itakapotajwa