- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: WATU MILIONI 3 KENYA WAKABILIWA NA NJAA
IDADI ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa nchini Kenya imefikiwa watu milioni 3.1 kwa mwaka huu 2022, idadi hii ya watu imeongezeka kutoka watu milioni 2.8 kwa mwaka jana 2021 ikiwa ni ongezeko la watu 300,000 kuanzia Desemba 2021 hadi Januari 2022, kulingana na ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Ukame Nchini Kenya (NDMA).
Jumla ya watu 2.8 milioni walikuwa wakikabiliwa na njaa kufikia Desemba 2021 lakini idadi hii imepanda hadi kufikia 3.1 milioni kufikia mwishoni mwa Januari 2022.
Uchuguzi huo kuhusu utoshelevu wa chakula uliendeshwa na asasi hiyo ya serikali kwa ushirikiano na washirika wa kimaendeleo wakiongozwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP).
“Kati ya watu 3.1 milioni wanaohitaji misaada ya chakula kwa dharura, 500,000 ni watu wanaochukuliwa kama wale walioko katika awamu hatari huku 2.6 milioni waliosalia wakiwa katika awamu ya pili ya hitaji la chakula,” NDMA ikasema katika taarifa Jumanne.
Mamlaka hiyo ilisema uchunguzi huo kuhusu hali ya chakula ulifanywa kwa lengo la kubaini manufaa ya mvua fupi ya Oktoba hadi Desemba 2021 katika mpango mzima wa uzalishaji chakula na usambazaji wake haswa katika maeneo kame nchini.
Maeneo hayo ambayo huathirika haraka kutokana na mabadiliko ya hali ya anga na tabia nchi, ni kama vile: kaunti za Samburu, Turkana, Baringo, Marsabit, Wajir, Mandera, Garissa, Isiolo na Tana River. Maeneo kadha katika kaunti za Moyale, Kitui, Meru na Laikipia pia yanachukuliwa kama yanayoathirika na ukame na baa la njaa.
Ripoti hiyo pia inasema kuwa angalau watoto 656,000 wenye umri wa kati ya miezi sita na 59 wanaathirika na utapiamlo na wanahitaji matibabu ya dharura. Karibu akina mama 100,000 wajawazito na wanaonyonyesha pia wanaathiriwa na utapiamlo.
Mvua chache iliyoshuhudiwa kati ya Oktoba na Desemba 2021, athari za misimu ya nyuma ya mvua chache, kupungua kwa uzalishaji wa mimea na mifugo, kupanda kwa bei ya chakula, pia ni baadhi ya changamoto zilizotajwa kuchangia kero ya ukosefu wa chakula.
Visababishi vingine ni janga la Covid-19 na athari zake husika mapigano na utovu wa usalama kwa ujumla katika kaunti za Baringo na Marsabit.
Mnamo Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta alizindua shehena ya chakula cha msaada ambayo ilipaswa kusambazwa katika kaunti 23 zilizoathiriwa na ukame kwa manufaa ya watu 2.3 milioni.
Kiongozi wa taifa pia alitangaza kuwa serikali yake imetenga Sh2 bilioni kuzisaidia familia zilizoathirika na ukame pamoja na baa la njaa katika kaunti hizo.
“Pesa hizo zitasaidia katika ununuzi na usambazaji wa chakula cha msaada, usambazaji wa maji na ununuzi wa mifugo iliyoathirika,” akasema.