Home | Terms & Conditions | Help

April 3, 2025, 12:11 pm

NEWS: WANANCHI DODOMA WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA HATIFUNGANI YA MIUNDOMBINU YA BARABARA

DODOMA: Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani kutumia fursa ya kununua hisa zilizopo katika Hatifungani ya Miundombinu ya Barabara (Samia Infrastructure Bond) kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara za wilaya zinazosimamiwa na TARURA.

Ametoa wito huo wakati wa utoaji elimu ulioenda sambamba na zoezi la uuzaji hisa za hatifungani hiyo kwa wadau mbalimbali wa mkoa wa Dodoma na mikoa jirani katika ukumbi wa Mabele mkoani Dodoma.

“Ni mara chache sana kukutana na kujadili fursa za uwekezaji, jambo hili ambalo ni muhimu kwenye maisha yetu tumekuwa hatulipi kipaumbele, leo hii serikali na taasisi binafsi zinaungana katika suala la maendeleo ya nchi yetu, CRDB na TARURA wametukutanisha hapa ili tuwekeze katika Hatifungani ya Samia katika ujenzi wa barabara, naamini mapato yatakayopatikana ya mauzo ya hatifungani hii yatasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi ya barabara nchini hivyo nawasihi watu wengi tujitokeze kuwekeza katika hatifungani hii”.

Katika hafla hiyo, Mhe. Senyamule alikusanya shilingi Bilioni 1.5 kutoka kwa wadau mbalimbali ambapo ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuwekeza katika hatifungani hiyo ambayo faida yake inatoa riba ya asilimia 12 kwa mwaka, inayolipwa kila robo mwaka ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Amesema hatifungani hiyo ina lengo la kukusanya fedha zitakazowasaidia wakandarasi wazawa ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa wakati lakini inatoa fursa kwa wawekezaji kupata faida kutokana na fedha wanazoweka yaani unashiriki kujenga nchi huku unapata faida kutokana na mtaji uliowekeza, amefafanua Mhe. Semanyule.

Kwa upande wake, Vivian Komu Mwenyekiti wa Bodi wa Wakandarasi mkoani Dodoma amesema wao fedha hizo za hatifungani ya miundombinu ya Samia zitawasaidia wakandarasi kutekeleza majukumu yao ya miradi hasa wakati ambao serikali inakuwa haina fedha.

Hatifungani ya Samia inatolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kufadhili miradi muhimu ya miundombinu nchini ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 150 kinatarajiwa kukusanywa kupitia Hatifungani hiyo kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara chini ya TARURA ili kuongeza mtandao wa barabara za vijijini na mijini, kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara unafanyika kwa wakati na kusaidia kukabiliana na mahitaji ya dharura ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu unaosababishwa na uharibifu wa mvua kubwa na mafuriko.