Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 3:55 pm

NEWS: WANACHUO 13 MBARONI KWA UDANGANYIFU

Dodoma.Wanafunzi 13 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dodoma, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wa mitihani ya marudio(SAP).

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alisema wanafunzi hao wa mwaka wa tatu 2020 wanashikiliwa kwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa marudio somo la Applied Statistics II uliyofanyika Novemba mwaka jana kwa mwaka wa tatu.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na taasisi hiyo unaonesha kwamba wanafunzi hao walitumia rushwa kupata mitihani hiyo ili warudie nje ya chumba cha mitihani karibu na chuo hicho.

Baada ya kufanya mitihani hiyo nje ya chumba cha mitihani karibu na chuo hicho, wanafunzi hao walijaribu kuingiza katika mfumo rasmi karatasi za matokeo walizotumia kujibia mitihani hiyo ndipo chuo kikabaini ujanja huo na kuripoti Takukuru.

"Wanafunzi hao walitaka kuingiza makaratasi ya mitihani hiyo kwenye mfumo rasmi wa matokeo ya chuo kwa kuchomoa karatasi walizofanya kwanza, ndipo chuo kikabaini na kuripoti Takukuru," alisema Kibwengo.

Kibwengo alisema, kutokana na tuhuma hizo wanazokabiliwa nazo wanafunzi hao, Takukuru inawatafuta waliomaliza masomo yao miaka ya nyuma lakini wapo mazingira nje ya chuo. Aliwataja wanafunzi wawili kuwa wanaonekana ndio viunganishi wa mbinu hizo.

Alisema wanafunzi hao wanatakiwa kuripoti mara moja katika ofisi za Takukuru mkoani Dodoma kwa ajili ya kusaidia uchunguzi wa nani alitoa mitihani chuoni hapo kwa wanafunzi hao.