Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 7:16 pm

NEWS: WALIOZIACHA HATI ZAO ZA ARDHI WIZARANI KUTOZWA KODI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kuanzi Julai Mosi mwaka huu wananchi wote wasiochukua hati za ardhi huku maeneo yao yakiwa yamepimwa na michoro yake kuidhinishwa wataanza kudaiwa kodi ya pango la ardhi.

Hatua hiyo inafuatia Bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria inayomtaka mwananchi aliyepimiwa ardhi na michoro kuidhinishwa kuchukua hati katika kipindi kisichozidi siku tisini na asipofanya hivyo ataanza kudaiwa kodi ya ardhi.

Akizungumza na wananchi mkoani Njombe jana wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya ardhi ya mkoa huo, Naibu Waziri Mabula alisema, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wamiliki wa ardhi kukwepa kuchukua hati za ardhi wakati taratibu zote zikiwa zimekamilika ikiwemo kuidhinishwa michoro na kuwekewa alama za mawe.

Alisema, pamoja na wananchi wakiwemo wa Njombe kufurahia usogezwaji huduma za sekta ya ardhi karibu lakini ni lazima wawajibike kwa kulipa kodi ya ardhi na kupatiwa hati aliyoieleza kuwa inaongeza thamani ya ardhi sambamba na hati miliki yake kutumika katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, amezitaka ofisi za ardhi katika halmashauri zote nchini kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo yao kuhusiana na umuhimu wa kuchukua hati ili kujua takwa la kisheria hasa ikizingatiwa wengi wao wameshindwa kuchukua hati kwa sababu mbalimbali.

Akiegeukia uchukuaji hati za ardhi kwa mkoa wa Njombe, Dkt Mabula alisema mkoa huo una jumla ya hati 42,516 zilizoidhinishwa lakini kati ya hizo ni hati 11,246 tu ndizo wamiliki wake walijitokeza kuzichukua huku wamiliki 31,270 wakiwa hawajachukua.