Home | Terms & Conditions | Help

December 3, 2024, 8:59 pm

NEWS: WADHAMINI WA LISSU MATATANI, MAHAKAMA YATOA HATI YA KUWAITA

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam , imetoa hati ya kuwaita mahakamani wadhamini wa aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania (Chadema),Tundu Lissu, na wanahitajikia kufika mahakamani hapo Januari 25, 2021.

Mahakama inawataka Wadhamini hao kufika mahakamani hapo ili wajieleze sababu haswa za kushindwa kufika mahakama na kwanini wameshindwa kumpeleka Lissu mahakamani hapo kama sheria inavyowataka.

Hatua ni baada ya mshtakiwa huyo pamoja na wadhamini wake kushindwa kufika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake ya jinai namba 233/2016 iliyopo mahakamani hapo.

Hii ni mara ya tano, kwa Lissu kushindwa kufika mahakamani hapo kuhudhuria kesi zake, tangu aliporejea nchini Julai 29,2020, akitokea nchini Ubeljiji alipokuwa anapatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajafahamika.

Jana, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliieleza Mahakama hiyo mbele ye Hakimu Mwandamizi, Rashid Chaungu kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya uamuzi kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la, lakini mshtakiwa na mawakili wake hawakuwapo mahakamani.

“Kutokana na mshtakiwa pamoja na wadhamini wake kushindwa kufika mahakamani hapa bila taarifa, tunaomba mahakama itoe hati ya kuwaita wadhamini wa Lissu wafike mahakamani hapa ili kesi yake iweze kuendelea, kwa sababu imeshindwa kuendelea kwa muda mrefu sasa” alidai wakili Simon.

Hakimu Chaungu, baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alikubaliana na ombi hilo na kutoa hati ya kuwaita wadhamini wa Lissu wafike mahakamani hapo Januari 25, 2021 itakapotajwa.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la kutoa maneno ya uchochezi katika kesi ya jinai 233/2016. Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo, Juni 28, 2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kwa lengo kuleta chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa maneno ya uchochezi ambayo yanasomeka kama ifuatavyo


“Mamlaka ya Serikali mbovu ya Kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila mtanzania kwa nguvu zote,huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanyanywa na utawala wa kijinga nchi itaingia ndani ya giza nene”