Home | Terms & Conditions | Help

December 4, 2024, 10:44 am

NEWS: VIWANGO VYA JUU VYA HUDUMA, UADILIFU, UBUNIFU NI MAONO YA AAAG_ DKT. NCHEMBA

ARUSHA: Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa viwango vya juu vya huduma, uadilifu na ubunifu ni sifa za uongozi ambazo zinaendana na maono ya Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Serikali wa Afrika (AAAG).

Ameyasema hayo jana Desemba 02, 2024 jijini Arusha wakati akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa kufungua Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Afrika (AAAG) kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Waziri Dkt. Nchemba amesema kuwa kuwepo kwa viongozi wakubwa katika mkutano huo ni ishara ya umuhimu mkubwa kwa viongozi wa nchi katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma, kuhakikisha uwajibikaji katika kila ngazi na kuendeleza dhana ya uwazi barani Afrika.

"Uongozi huu unatuvutia na kutupa msukumo wa kufuata viwango vya juu vya huduma, uadilifu na ubunifu, sifa ambazo zinaendana na maono ya Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Serikali wa Afrika. Tunamshukuru sana Rais Samia na nyie wasaidizi wake kwa kutuheshimisha kupitia maono yenu yanayotutia moyo na kuhamasisha juhudi zetu", alisema Dkt. Nchemba.

Amefafanua kuwa, mkutano huo una wajumbe mashuhuri miongoni mwao ambao wanawakilisha hazina ya uzoefu, uaminifu na maono ya kimkakati yanayohitajika katika kukabiliana na changamoto ngumu za kifedha zinazozikabili nchi za Afrika.

"Michango yenu inatoa mwanga wa matumaini kwa juhudi zetu za pamoja za kujenga msingi imara kwa maendeleo endelevu ya bara letu." Alimalizia Dkt. Nchemba.

Leo ni siku ya pili ya mkutano huo unaofanyika kwa siku nne (4) jijini humo. Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Kujenga Imani ya Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu” umehudhuriwa na washiriki takribani 1,800 kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania.