Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 7:46 am

NEWS: UTEUZI WA DPP BISWALO KUWA JAJI WAZUA UTATA, WAPO WALIOFURAHIA

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo May 11, 2021 amefanya uteuzi wa majaji 7 wa mahakama ya rufani na majaji 21 wa mahakama kuu ya Tanzania ndani ya Teuzi hizo yupo Biswalo Mganga aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Mashtaka nchini(DPP).

UTEUZI WA BISWALO KISHERIA

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serekali DPP kwa mujibu wa sheria anakoma kuwa kwenye nafasi yake hiyo katika mazingira makuu matatu muhimu.

1. Akistaafu kwa mujibu wa Sheria, kifungu namba 20 NPS Act

2. Akijiuzulu kwa mujibu wa kifungu cha 21 NPS Act.

3. Au kwa kuondolewa na Rais mara baada ya kupata mapendekezo kutoka kwenye tume atakayounda kuchunguza mienendo yake.

Sheria hii ya NPS Act inasema taratibu za kumwondoa DPP madarakani zinafanana na zile za kumwondoa Jaji wa Mahakama Kuu, Madarakani.

Sheria inataka Rais aliyopo madarakani aunde Tume maalumu ambayo ikamchunguze DPP na mara baada ya kuchunguza itatoa mapendekezo ya kama DPP aondolewe katika nafasi yake au aendelee kufanya kazi kwa kuwa yupo salama(msafi).

MASWALI YA KISHERIA.

Sasa leo Jumanne May 11, 2021 Bw. Biswalo Mganga ambaye ndio DPP wa Tanzania ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, kwa maana hiyo amekoma kuwa DPP leo, Sasa Maswali ni Je? Rais aliunda tume kufanya kazi ya kuchunguza mienendo yake kwa mujibu wa sheria na Je tume hiyo iliundwa lini na mapendekezo yake yakoje?.

WALIOFURAHIA KUONDOLEWA KWAKE.

Bw. Bishwalo Mganga aliteuliwa na Rais wa awamu ya Nne Jakaya Kikwete kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini Siku ya Jumanne Octoba 6, 2014 na baadae akaendelea kushika wadhifa huo chini ya Hayati Rais John Magufuli.

Wakosoaji wengi wakiwemo wanaharakati wa kisheria na haki za kibinaadamu walimkosoa vikali Bw. Biswalo Mganga, katika nafasi yake kama DPP, wengi wao wakisema kuwa kupitia yeye, Sheria nyingi kandamizi zimeundwa, ikiwemo sheria ya uhujumu uchumi na Sheria ya Plea Bargain ambayo DPP anakaa meza moja na mtuhumiwa wa uhalifu au Mbadhirifu analazimishwa kukubali kosa na kukubaliana kiwango cha fedha kufidia.

Nyingine Wanadai kuwa Mganga alitumika kwenye operesheni ya kuzifungia na kuyafilisi makampuni ya kubadilishia fedha za kigeni (Bureau De Change).

Pia ofisi ya DPP imekuwa inamatendo ya ucheleweshwaji wa kesi kwa kisingizio cha upelelezi bado haujakamilika, hatua ambayo imewaumiza watu wengi, wakiwemo viongozi wa Vyama vya Siasa nchini walipokuwa na kesi mahakamani.

Kwa hiyo wadau hao wanahisi kuwa Huenda kuondolewa kwake kwenye nafasi hiyo ya DDP kunaashiria mwanzo mpya wa Haki nchini, huku wengine wakidai kuwa haki haiwezi kupatikana mapaka sheria zote kandamizi zifutwe.

Imeandaliwa na Deyssa H. Issa

na Kuhaririwa na Merry Mgawe

Muakilishi Publisher

Leo May 11, 2021.