Hali hii huzifanya picha za ngono kuwa biashara namba tatu inayowaingizia baadhi ya matajiri duniani mabilioni ya dola ikiwa nyuma ya biashara ya dawa za kulevya na kamari.
Kutokana na ukweli kwamba picha hizi zinaangaliwa katika mazingira ya faragha, zimekuwa kivutio kwa watu wengi wanawake na wanaume hasa vijana.
NINI MADHARA YA KUTAZAMA PICHA ZA NGONO
Kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, Dk Judith Gelernter Reisman ambaye ni profesa wa utafiti katika Chuo Kikuu cha Liberty Marekani, alizipatia picha hizi jina la “erototoxin,” akimaanisha kuwa zina uwezo wa kudhuru ubongo wa mtu anayezitazamani kwa muda mrefu.
Dk Reisman alibainisha kuwa vichocheo vya kemikali za mwili vinavyozalishwa kwa wingi na kusisimua neva kupita kiasi wakati wa kuangalia picha hizi, vina athari mbaya kwenye ubongo.
Kutokana na athari zake, watu wengi duniani kote wametekwa na mawazo ya ngono kuliko kitu chochote.
Katika utafiti uliofanywa na Terri Fisher pamoja na wenzake kutoka Chuo Kikuu cha Ohio (OSU) nchini Marekani na kuchapishwa mwaka 2012 katika jarida la utafiti wa masuala ya ngono (Journal of Sexual Research) toleo namba 49(1), ilibainika kuwa wanaume wengi siku hizi hufikiria tendo la ngono kwa wastani wa mara 19 kila siku, wakati wanawake wakifikiria ngono kwa wastani wa mara 10 kwa siku.
Katika utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2008 na kupewa jina la “Generation XXX,” watafiti pia walibaini kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi wengi vijana katika vyuo vikuu huko Marekani, wanaamini kuwa kuangalia picha za ngono ni jambo linalokubalika kimaadili. Utafiti huo pia ulibainisha kuwa wavulana tisa kati 10 na msichana mmoja kati ya watatu ni watazamaji wa picha za ngono.