Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres huku akisema umoja huo hautounga mkono hatua ya kuiwekea tena Iran vikwazo, kama ambavyo Marekani inataka hadi hapo atakapopewa idhini na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika barua aliyomuandikia rais wa baraza hilo na kuonekana na shirika la habari la AP, Guterres amesema kuna hali ya sintofahamu iwapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ameanzisha mchakato au la wa kurejesha vikwazo katika azimio la Baraza la Usalama ambalo lilitia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani.
Siku ya Jumamosi serikali ya Rais Donald Trump ilitangaza kuwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa, hatua ambayo imepingwa na mataifa mengine duniani yakisema havina uhalali na vinafaa kupuuzwa.