Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 4:25 pm

NEWS: TUME YAKUBALI RUFAA ZA WABUNGE ZINGINE 13

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekubali rufaa 13 na kuwarejesha wagombea ubunge katika orodha ya wagombea baada ya kuchambua na kuzifanyia uamuzi furaa za wagombea ubunge kutoka majimbo tisa zilizowasilishwa na wagombea kupitia kwa wasimamizi wa uchaguzi nchi nzima.

Akitoa taarifa kwa umma Jana Septemba 9, 2020 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Dkt. Wilson Mahera Charles amesema uamuzi huo umetolewa katika kikao cha Tume cha jana tarehe 08 Septemba 2020 baada ya kuzipitia, kuchambua na kuzifanyia uamuzi rufaa 34.

Dkt. Charles ameyataja majimbo ambayo wagombea hao wamerejeshwa kuwa ni majimbo ya Singida Magharibi, Madaba, Ilemela, Namtumbo, Bagamoyo, Liwale, Tunduma, Bukene na jimbo la Kigamboni.

Katika hatua nyingine, Dkt. Charles amesema Tume imekataa rufaa 8 za wagombea ambao hawakuteuliwa kutoka kwenye majimbo ya Singida Magharibi, Bahi, Handeni Vijijini, Madaba, Singida Mashariki, Ileje, Meatu, Kisesa na Bukene.

“Tume imekataa rufaa 13 za kupinga walioteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka kwenye Majimbo ya Mwanga, Mafinga, Ilala, Manonga na Igunga”, ameongeza Dkt. Charles.

Dkt. Charles amesema idadi ya rufaa hizo 34 inafanya jumla ya rufaa za wagombea ubunge zilizofanyiwa uamuzi na Tume kufikia rufaa 89 kutokana na rufaa 55 zilizotangazwa juzi na Tume.

Amesema Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kila siku na kwamba wahusika wa rufaa hizo wameanza kujulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume kuanzia leo.

Rufaa hizo zimewasilishwa chini ya kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ambacho kinatoa fursa kwa wagombea wa ubunge kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa.