Home | Terms & Conditions | Help

April 5, 2025, 2:26 am

NEWS: TUME YA UCHAGUZI KENYA KUCHUNGUZA MADAI YA RUTO KUIBIWA KURA

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini Kenya(IEBC) inajiandaa kumpelekea barua ya wito Naibu Rais wa Kenya Dkt William Ruto ili afike mbele ya Tume hiyo kwa ajili ya kujieleza kutokana na madai aliyoyatoa ziarani nchini Marekani kuwa kuna mipango ya kuiba kura zake katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti 9.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume hiyo itachunguza madai hayo kama sehemu ya mikakati yake ya kuhakikisha kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki.

“Binafsi sijapata maelezo ya kina kuhusu madai aliyoyatoa Naibu Rais Dkt William Ruto akiwa Marekani.

Baada ya kupata maelezo, IEBC itachunguza madai hayo kisha kutoa ufafanuzi kwa Wakenya,” akasema Bw Chebukati akiwa jijini Nakuru.

“Wawaniaji wote wa urais wanafaa kutii sheria. Tutachunguza suala hili na kuwaeleza Wakenya kuhusu madai ya wizi wa kura,” akaongeza Mkuu huyo wa IEBC.

Alizungumza baada ya IEBC kutia saini mkataba na washikadau katika sekta ya uanahabari wa jinsi ya kufuatilia matukio kabla wakati na baada ya uchaguzi huo. Hasa mkataba huo utajikita katika kuhakikisha vyombo vya habari vinaeneza kwa kuchapisha au kutangaza habari zilizothibitisha kuhusu uchaguzi huo.

Dkt Ruto alitoa madai kuwa kuna mipango ya kushiriki udanganyifu mnamo Jumanne akiwa Marekani ambapo alitoa wito kwa umoja wa

mataifa uingilie kati na kuzuia jaribio la udanganyifu katika uchaguzi huo.

Hasa Naibu Rais alisema kuwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inahusika kwenye mpango huo wakati akitoa hotuba yake katika Chuo Kikuu cha Loyola, Maryland. Alithibitisha madai yake kwa kudai kuwa idara mbalimbali za serikali sasa zinatumika kuwatishia na kuwakandamiza viongozi wanaomuunga mkono.

Dkt Ruto anayeongoza muungano wa Kenya Kwanza na Chama cha UDA, atakabiliana na Kinara wa ODM Raila Odinga wa vuguvugu la Azimio la Umoja miongoni mwa wagombeaji wengine katika uchaguzi huo.

Madai kuwa kuna mipango inayoendelea ya wizi wa kura yaliyotolewa na Dkt Ruto hata hivyo yalijibiwa vikali na wandani wa Bw Odinga ambao walisema hiyo ilikuwa ishara kuwa Naibu Rais alikuwa ametambua atashindwa katika uchaguzi huo.