Tanzania imepokea shehena milioni 1 ya kwanza ya chanjo ya corona ya Johnson and Johnson iliotolewa na Marekani.
Marekani imetoa msaada huo kupitia mpango wa usambazaji wa chanjo wa COVAX kwa uratibu wa Umoja wa Afrika. "Hiki ni Kielelezo cha uimara wa ubia wetu wa miaka 60 na dhamira yetu ya dhati kwa Tanzania" ilisema sehemu ya taarifa ya Marekani.
Chanjo hizo zimepokelewa na Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Liberata Mulamula na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Tanzania ni moja ya mataifa ambayo yalikuwa bado hayajapokea chanjo barani Afrika, au hata kuanza kuchanja watu baada ya kiongozi wake wa zamani , John Pombe Magufuli, kukataa chanjo hizo na kudai kuwa taifa hilo limeushinda ugonjwa wa COVID-19.
Samia Suluhu Hassan, aliechukua nafasi ya rais baada ya kifo cha Magufuli, amebadilisha dhana ya kukataa kuwa Tanzania hakuna corona.