Home | Terms & Conditions | Help

November 10, 2024, 10:44 pm

NEWS: TANESCO YAENDELEA KUSHUSHA NEEMA KWA WANANCHI.

KONDOA: Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Dodoma limeendelea na zoezi la uelimishaji na uhamasishaji katika vijiji vinavyonufaika na miradi ya umeme inayoendelea Wilayani Kondoa kupitia wakala wa Nishati vijijini REA.

Elimu hiyo kwa umma imehusisha kufahamisha wananchi juu ya miradi ya REA na utekelezaji wake, uepukaji vishoka pamoja na matumizi sahihi ya umeme wenyewe ikiwemo uzingatiaji wa usalama kwanza.

Akiongea katika vijiji vya Kikilokati, Berabera na Kwahengwa kata ya Kikilo, Kondoa Mkoani Dodoma, Afisa uhusiano Sarah Libogoma amewataka wananchi kupokea mradi unaoendelea kwenye maeneo yao kwa kuhakikisha wote waliofikiwa na awamu hii wanajitokeza kuomba huduma kadri serikali ilivyokusudia kwani gharama za mradi huo zimepunguzwa sana kwa Mwananchi.

"Kwa shilingi 27,000 unakuwa umepata huduma kwa pesa ambayo ukiuza kuku wawili unaunganisha huduma ya umeme milele kwenye nyumba yako hivyo ni vyema kuhakikisha tunatumia fursa hii vizuri kwani mradi upo ukingoni kukamilika." Alisema Libogoma

Pia wananchi wamehimizwa kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza kipindi chore cha mradi na kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka za serikali zilizopo katika maeneo yao.

Aidha, wananchi wametakwa kuzingatia usalama katika matumizi ya umeme ikiwamo, kutofanya shughuli zote chini au karibu na miundombinu ya umeme kama vile Transfoma, kuhakikisha wanatumia mafundi wanaotambulika katika 'Wiring' ya nyumba zao pamoja na kutokata miti iliyo karibu na nyaya za umeme bila kushirikiana uongozi ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Hata hivyo Libogoma kupitia uhamasishaji huo katika vijiji vyote ameendelea kusisitiza utunzaji wa miundombinu ya umeme kwani serikali inatumia gharama nyingi katika kupeleka miradi katika maeneo hayo kwa manufaa ya wananchi wake wote hivyo ulinzi ni shirikishi.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kikilo Yuda Daniel ameishukuru Serikali kwa kupeleka miradi hiyo kwakuwa kilikuwa kilio kikubwa kwa wananchi wapate umeme huku akisisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili kufanikisha miradi hiyo.

“Wananchi wanamatumaini makubwa na Serikali yao hivyo naamini watatoa ushirikiano wa kutosha kwani wamefurahia mno kufikiwa na mradi huu,”

Nao wananchi wa vijijini hivyo akiwemo Hamisi Said wa Kijiji cha Kwahengwa na Karimu Msondo wameishukuru serikali nakuiomba kwa vile vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme basi Serikali ivikumbuke.

Uhamaishaji huu imefanywa na TANESCO kea kushirikiana na Mkandarasi Ok Electrical anayetekeleza mradi huo kwenye vijiji wilaya za Kondoa na Mpwapwa ambapo ameshatekeleza takribani asilimia 50 ya mradi huo.

Mradi huu unatarajia kumalizika January 2023 , ambapo katika Wilaya ya Kondoa Kati ya Vijiji 34 ,Vijiji 14 tayari vimewashwa , huku Kazi ya kuwasha ikiendelea katika vijiji 20 vilivyobakia.