- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: TAASISI ZISIZOJISAJILI KUCHUKULIWA HATUA
DODOMA: Serikali imetangaza kuwa kuanzia tarehe 1 Mei 2025, Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kwa kushirikiana na vyombo vya utekelezaji wa sheria itaanza kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya taasisi zote ambazo zitabainika hazijasajiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema kuwa kwa mujibu wa vifungu vya 14 na 21 vya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Na. 11 ya mwaka 2022, taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya, kuchakata, au kuhifadhi taarifa binafsi zinawajibika kusajiliwa na Tume hiyo ili kuhakikisha ulinzi wa taarifa za wananchi.
Amesema, ili kutoa nafasi ya mwisho kwa taasisi ambazo bado hazijakamilisha usajili wao, Dkt. Mkilia amesema kuwa taasisi hizo zina hadi tarehe 30 Aprili 2025 kukamilisha mchakato wa usajili. Baada ya muda huo, taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu huo zitachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini na adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria
Dkt. Mkilia amesisitiza kuwa kulinda taarifa binafsi siyo tu hitaji la kisheria, bali pia ni kiashiria cha uwajibikaji wa taasisi na dhamira ya kulinda haki za wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 16(1), inayotoa haki ya faragha kwa kila mwananchi.
Katika hatua nyingjne Dkt. Mkilia amesema kuwa uzingatiaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya ajenda ya mabadiliko ya kidijitali nchini. Alihimiza taasisi zote kuzingatia muda uliowekwa na kuchukua hatua zinazohitajika ili kuendana na viwango vya kimataifa vya usalama wa taarifa binafsi.
Kwa hatua hii, Tanzania inalenga kuweka mifumo thabiti ya ulinzi wa taarifa binafsi, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kidijitali, ulinzi wa haki za wananchi, na kuimarisha uwajibikaji wa taasisi za umma na binafsi.
Ikumbukwe kuwa wakati wa uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa agizo la kuhakikisha taasisi zote za umma na binafsi zinawasilisha usajili wao kama sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi nchini.