Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 12:34 pm

NEWS: SPIKA TULIA AMBANA KOO WAZIRI WA FEDHA KUHUSU MAKINIKIA

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackoson amemtaka waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba kumjibu kwa kadri alivyouliza Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina swali lake la msingi la ni kwanini Serikali ilikubali kupokea Sh700 bilioni zilizotokana na kesi za malimbikizo ya madeni ya makinikia badala ya Sh360 trilioni ambayo ni madai halali kwa Tanzania.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya Sakata la makinikia kuibuliwa Bungeni leo Alhamisi Septemba. 22, 2022, na mbunge huyo wa Kisesa Luhaga Mpina kuuliza swali hilo la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu.

“Kwa nini Serikali ilikubali kupokea Sh700 bilioni kutoka katika kesi za malimbikizo ya madeni maarufu kama makinikia badala ya Sh360 trilioni ambayo ni madai halali katika nchi yetu,”amehoji.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali haijakubali kupokea fedha hizo (Sh700 bilioni) na kuacha Sh360 trilioni, isipokuwa ilipeleka malalamiko kuhusu kampuni za madini.

Hata hivyo, kabla ya kumaliza kulijibu swali hilo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimkatisha na kutaka ufafanuzi wa majibu ya Serikali yaliyotofautiana na swali la msingi lililoulizwa na Mpina.

Akijibu swali hilo, Waziri Mwigulu amesema Serikali haikupokea kimya kimya fedha hizo (Sh700 bilioni) na kuacha Sh360 trilioni bali kilichofanyika ni kwa Serikali kupeleka malalamiko kwenye kampuni za madini.

Lakini kabla ya kuendelea kujibu, alikatishwa tena na Dk Tulia akimtaka kwenda kwa mtiririko huku akimtaka Waziri huyo kueleza juu ya tofauti ya fedha zilizoandikwa katika jibu la Serikali na zilizotamkwa na mbunge ili aweze kutoa mwongozo.

Akitoa ufafanuzi, DK Mwigulu amesema Sh360 trilioni anazozungumzia Mpina ni za makinikia wakati katika jibu la swali la msingi, kiasi kinachozungumziwa cha Sh4.21 trilioni ni za mashauri mengine ya kodi.

Baada ya maelezo hayo, Dk Tulia aliitaka Serikali kumjibu Mpina tena kwa kadri alivyouliza swali lake la msingi.

Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu amesema Sh360 trilioni haipo kwenye Bodi ya Rufani ya Kodi (TRAB) wala Baraza la Usuluhishi la Mapato ya Kodi (TRAT).

Amesema rufaa za kikodi ni mahususi na lilikuwepo kwenye mzozo wa Serikali na Kampuni ya Barick kwahiyo ni kitu tofauti.

Katika swali la msingi, Mpina amehoji nini kinachosababisha kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Sh360 trilioni na Dola za Marekani milioni 181.4 kutoamuliwa hadi sasa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande amesema

hadi Agosti 2022, kulikuwa na idadi ya mashauri 854 kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji, yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya Sh4.21 trilioni na Dola za Marekani Milioni 3.48 katika taasisi za rufani za kodi ambazo ni TRAB na TRAT.

Amesema hivyo, kwa sasa TRAB na TRAT zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa.

Aidha, amesema kwa nyakati tofauti, idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili.