Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 6:53 pm

NEWS: SPIKA TULIA AAGIZA KUFUTWA MANENO YA WAZIRI MABULA

Dodoma. Spika wa Bunge, wa Tanzania Dk Tulia Akson leo Alhamisi ametoa mwongozo wa Bunge kuhusu maneno aliyoyatumia Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula ya kumvaa mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi kuwa hayakuwa sahihi.

Spika Tulia ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 23,2022 kuwa lugha iliyotumiwa na Waziri huyo inamdharirisha mbunge na kumpa usumbufu kwa wananchi wake, hivyo akaagiza maneno yaliyotamkwa na Waziri Mabula yaondolewe kwenye kumbukumbu sahihi za Bunge.

Waziri Mabula aliliambia Bunge kwamba Kunambi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jijini la Dodoma, alisababisha migogoro mikubwa ya ardhi iliochangia kuongezeka kwa dhuruma za ardhi kwa wananchi.

Mabula alitoa kauli hiyo wakati akiomba kumpa taarifa mbunge Kunambi kwenye mchango wake ambao ulikuwa ukielezea namna ambavyo Serikali inaweza kupata mapato kwa kupima ardhi.

Kunambi pia alizungumzia mbinu alizotumia kwa kupima ardhi ya jiji akitaka iigwe na serikali ambayo ingemaliza kazi ya kupima ardhi kwa muda mfupi. Lakini baada ya kuelezwa hayo aliomba mwongozo kwa Spika iwapo kauli ya Waziri Mabula inakubalika.

Leo Spika ameeleza kwakirefu kuhusu kilichotokea na kusema Kunambi alikuwa sahihi kutoa kauli hiyo kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya ushauri ambao Serikali ingeweza kuuchukua au kuupuuza lakini si kujibiwa kama ilivyotokea.

Ameonya kuhusu matamshi yanayotolewa ndani ya Bunge kwamba yanaweza kuwaumiza wengine kwa kuwa kumbukumbu za Bunge zinadumu.