Home | Terms & Conditions | Help

April 4, 2025, 7:37 am

NEWS: SPIKA NDUGAI AMUONYA NAPE KUITA WABUNGE WENZAKE COVID19

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai amemuonya vikali Mbunge wa Mtama Nape Nnauye kwamba awe makini wakati anapochangia michango yake bungeni hasa wakati anapowazungumzia wabunge wanawake.

Spika ameoneshwa kukasirika kwake mara baada ya kudai Nape amewaita wabunge 19 wa Viti maalumu waliovuliwa Uwanachama na Chama chao cha Chadema kuwa ni Covid19 na wanapaswa kuondolewa bungeni kwa sababu ya kuvuliwa kwao uwanachama.

“Mdogo wangu Nape yalimtoka maneno kidogo na yamesambaa sana huko mitandaoni, ikifika mahali Spika na Mbunge mnapishana si jambo jema, yeye ana uhuru wa kusema lakini hana uhuru wa kuwasema wabunge wenzake, nilizungumza nae na ninawaomba mumsamehe, aliwakosea sana na ninaomba sana tuchunge midomo yetu.” Alieleza Spika Ndugai

Ndugai ametoa onyo hilo hii leo May 3, 2021 wakati aliposimama bungeni kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa likiwemo uwepo bungeni wa Wabunge 19 wa Viti Maalum kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo pamoja na kauli alizozitoa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kuhusiana na uwepo wa Wabunge hao Bungeni

Aidha Spika Ndugai amesema pamekuwa na maneno mengi ya kumshambulia kwenye mitandao ingawa yeye hapendi kushughulika na mambo ya mitandao. Ameeleza kuwa wengi wamekuwa wakilisifu Bunge la Tisa lililokuwa chini ya Spika Sitta lakini hawafahamu yeye alikuwa msaidizi wa karibu wa Spika Sitta akihudumu kama Mwenyekiti wa Bunge na ameshiriki kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza kanuni za Bunge zinazotumika sasa.

Hivi karibuni Nape alikosoa wabunge hao kuendelea na nafasi zao licha ya kufukuzwa Chadema, akitaka katiba ya nchi ifuate kumaliza hatima ya wabunge hao.

Spika Ndugai amemaliza kwa kuwataka Wabunge 19 wa Viti Maalum CHADEMA waendelee kuchapa kazi huku akisisitiza kwamba ana uzoefu wa kutosha na wanaosema amevunja katiba, hawajui wasemalo kwani yeye hawezi kufanya maamuzi kwa kuandikiwa kipeperushi bali ametaka Katibu wa CHADEMA aandike barua ikiambatanishwa na Katiba ya chama pamoja na muhtasari wa kikao kilichofanya maamuzi.