Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 8:27 pm

NEWS: SHAHIDI WA SEREKALI AELEZA ALIVYOPEWA KAZI YA MBOWE

Dar es salaam. Leo katika kesi ya kigaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Wenzake imeendelea kwa Mkaguzi wa Polisi Mahita Omary Mahita, kuielezea Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kuwa alipigiwa simu na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP, Ramadhaman Kingai, aende ofisi kwake.

Mahita ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, ameanza kutoa ushahidi wake leo Ijumaa Septemba 17, 2021, mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Septemba 15, 2021, upande wa utetezi walipinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Adam Kasekwa yasipokelewe na mahakama hiyo kwa sababu yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria na mshtakiwa huyo anadai kuwa aliteswa wakati anaandika maelezo yake kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Mahita ameieleza Mahakama hiyo kuwa yeye ni miongoni mwa askari Polisi ambao walifika Moshi Mkoani Kilimanjaro na kuwakamata washtakiwa Adam Kasekwa na Halfan Hassani.

" Baada ya kuwakamata washtakiwa Hawa tuliwaweka chini ya ulinzi nakuanza kuwapekua ambapo Adamu alikuwa na silaha aina ya bastola ilikuwa upande wa kushoto wa kiuno " amedai Mahita.

Shahidi huyo amedai anakumbuka Agost 4, 2020 alipigiwa siku na aliyekuwa RCO wa Arusha Ramadhani Kingai kwa kipindi hicho akimtaka afike ofisini kwake na yeye aliitikia wito.

" Baada ya kufika ofisi kwa Kingai, aliniambia kuna kazi ya kwenda kufanya Moshi alinieleza niandae askari wengine kwa ajili ya kazi hiyo" amedai Mahita ambaye kwa wakati huo alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi wilaya ya Arusha mjini na kuongeza.

“Niliandaa Askari hao na kisha safari ilianza ya kuelekea njia ya kwenda Kilimanjaro na kabla ya kuendelea na safari, tulisimama kituo cha Polisi Usariva kilichopo wilaya ya Arumeru na kukutana na SPJumanne na tukiwa katika kituo hicho mimi na Askari wenzangu, tulipewa maelezo kwa ufupi na ACP Kingai kuwa kuna kikundi kinapanga kufanya matukio ya kigaidi katika maeneo mbalimbali hapa nchini" amedai Mahita.

Shahidi huyo amedai kuwa vitendo hivyo vilipangwa kufanyika katika maeneo ya Moshi, Arusha, Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza.