Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 9:03 pm

NEWS: SEREKALI YAZIPA ONYO HOSPITALI BINAFSI ZINAZOPANDISHA GHARAMA ZA MATIBABU

Katibu mkuu Wizara ya Afya nchini Tanzania Prof. Mabula Mchembe ametoa onyo kali kwa hospitali za Binafsi zinazopandisha gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya upumuaji bila kufuata taratibu na miongozo ya ya Wizara ya Afya, huku akieleza kuwa, si kila tatizo katika mfumo wa hewa ni ugonjwa wa Corona.

Prof. Mchembe amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika hospitali kubwa za binafsi za Agakhan na Kairuki jijini Dar es saalam.

‘’Hilo suala ambalo nimeliona jana, na kwenye mitandao nimeona baadhi ya hospitali zingine wametoa makaratasi kuwa kwa wagonjwa anaonekana ana matatizo ya kupumua atalipishwa kiasi hiki, niziase pia hospitali, zisitumie nafasi hii, mtu kuwa na tatizo la kupumua kwenye mfumo wa hewa sio kwamba ana Corona, mbona mwanzo walivyokuwa wanawahudumia kabla ya haya yote haikuwa na gharama hizi, anasema Prof.Mchembe.

Aidha aliendelea kusisitiza kuwa hospitali hazijajaa wagonjwa wa Corona kama taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

"Sio kweli kwamba Hospitali hizi zimejaa wagonjwa wa Corona kama inavyosemekana kwenye mitandao ya kijamii, hospitali zina uwezo wa vitanda zaidi ya 150 lakini sio vyote vina wagonjwa na wapo wagonjwa wa kila aina wanaohitaji huduma", anasema Prof. Mchembe.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa hakuna maambukizi ya Covid-19 nchini Tanzania, lakini akiendelea kusisitiza kujilinda na kutumia dawa asili na kujifukiza.