Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 9:08 pm

NEWS: SEREKALI KUPUNGUZA UINGIZWAJI WA MAFUTA TOKA NJEE

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongeza nguvu kwenye uzalishaji wa zao la alizeti kwa lengo la kuhakikisha kuwa kuna mafuta ya kutosha ya kula yanayozalishwa nchini na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta hayo kutoka nje.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya kilimo nchini zinaeleza kuwa uzalishaji wa ndani wa mafuta ni asilimia 43 tu kwa jumla ya walaji nchini. Aidha nchi inazalisha tani 270,000 za mafuta ya kula kila mwaka na huagiza nyingine tani 600,000 ili kufidia pengo la asilimia 57% lililopo ndani.

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo Juzi Januari 22, 2021 wakati alipofanya ziara ya kukitembelea kiwanda cha kusindika mafuta ya kula ya alizeti; Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania cha Jijini Dodoma.

Prof. Mkenda amesema kwamba pamoja na kuongeza nguvu kuhakikisha kwamba mafuta ya kula yanapatikana nchini kwa kiasi kinachotakiwa pia serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwawezesha wawekezaji na pia wakulima wadogo kuwa nafasi ya kusafirisha bidhaa zao nje.

Prof. Mkenda amesema kwamba anafahamu kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanasababishwa kukwama kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini hivyo Serikali itapitia upya Sheria na kanuni ili kuondoa mkwamo na kuwezesha uzalishaji wa ndani kukua zaidi.

Waziri Mkenda alisisitiza kuwa hakuna mageuzi ya kiuchumi yanayoweza kutokea bila kuwa na mapinduzi kwenye kilimo.

"Tukiongeza tija kwenye kilimo, bei za bidhaa kama chakula itapungua, mageuzi kwenye kilimo yatasaidia sana kukuza viwanda hapa nchini.” Amesisitiza Prof. Mkenda.

Waziri wa Kilimo amesema suala la mbegu za alizeti ni changamoto lakini Serikaĺi itahakikisha mbegu za kutosha zinapatikana. Pia alitaka kuangaliwa kwa mfumo wa kilimo cha mkataba kwa kuboresha mfumo wake.

"Tabia ya Watu kuingia mkataba lakini wakati wa kuvuna wanampa mtu mwingine haipendezi, lazima Wakulima waheshimu mikataba.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa ataitisha mkutano wa Wataalamu ili kuangalia upya sera na taratibu zinazotumika katika uzalishaji wa alizeti nchini.

Hata hivyo alikiri kwamba mahitaji ya mafuta ya kula nchini yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa corona ambao umesababisha mwenendo usiokuwa wa afya wa biashara ya kimataifa ikiwamo ya mafuta ya kula.

Waziri pia aliwaambia Wamiliki wa Kiwanda cha Pyxus Agriculture Tanzania kwamba Serikali haijazuia upelekaji wa mafuta ya kula nje na kwamba kuchelewa kwa maofisa wa Serikali kutoa vibali kunaathiri Wakulima wadogo hapa nchini ambao wanategemea kiwanda kama hicho kupata soko la uhakika.

“Kiwanda hicho kimepata soko katika Jumuiya ya Ulaya ya kupeleka mafuta yaliyosafishwa mara mbili (Double Refined).”

“Tuna uwezo wa kuilisha nchi yetu na mafuta tunayozalisha wenyewe na kuuza mengine nje” alisema Profesa Mkenda na kuongeza kuwa kwa bahati mbaya Wakulima wadogo bado wanahangaika katika uzalishaji.

“Wataalam wanasema kama Wakulima wakibadilika na kufanya kilimo biashara chenye matumizi ya zana za kisasa na mbegu bora za kisasa wataweza kuzalisha tani 10 za alizeti kwa hekta.”

“Wakulima nchini wanazalisha chini ya tani moja kwa hekta.” Amekaririwa Waziri Mkenda