Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 2:15 pm

NEWS: SABAYA AHUKUMIWA MVUA YA MIAKA 30 JELA

ARUSHA. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake baada ya kukutwa na hatia ya katika Kesi ya unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo amesema kuwa ameridhika mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake na kuwatia hatiani kosa unyang’anyi wa kutumia silaha.

Baada ya kuwatia hatiani wakili wa Serikali amesema hakuna kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washtakiwa wote watatu, na kuiomba Mahakama iwape adhabu ya miaka isiyopungiua 30 jela na viboko.

Hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikimkabili Sabaya imesomwa leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.

Kabla ya kuanza kusomwa hukumu, Wakili wa Serikali, Felix Kwetukia aliweka wazi kuwa Jamhuri ipo tayari kupokea hukumu huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Moses Mahuna, Silvester Kahunduka na Wakili Fridolin Germelo nao walisema wapo tayari kusikiliza hukumu hiyo.

Hakimu Omworo amesema kuwa imethibitika mshitakiwa wa kwanza alikuwa na bastola ndani na nje kulikuwa na watu wawili wenye silaha hivyo, hakuna shaka duka la shahidi wa kwanza lilivamiwa na watu wenye silaha na lilikuwa chini ya watu wenye silaha.

Akisoma maelezo ya awali Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Odira Amworo amesema kati ya mashahidi 11 wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi wao, ambapo ushahidi wa watu 9 umeonekana una mashiko na ushahidi wa watu wawili umetupwa.

Hakimu Amworo amesema kuwa mahakama imejiridhisha kuwa siku ya tukio February 9 mwaka 2021 washtakiwa wote watatu walikua dukani kwa Saad na wote walishiriki kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha, kabla ya kumpiga Saad na kumsabanishia majeraha, wakitaka wapewe TZS 100M au mfanyabiashara huyo apewe kesi ya uhujumu uchumi.

Hakimu anasema kwa mujibu wa kifungu cha 201 cha sheria ya makosa ya adhabu, mtu yeyote anayepatikana na hatia ya kutumia silaha kunyang'anya mali ya mtu mwingine, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela pamoja na viboko 12 au miaka 30 bila viboko.

Baada ya kusema hayo Sabaya alianguka na kudaiwa kuzimia, hali iliyofanya Hakimu kuahirisha kusoma hukumu hiyo kwa dakika 5. Baadae Sabaya alizinduka na hukumu ikaendelea kusomwa.

Washtakiwa, Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani leo saa 3:05 asubuhi, kwa ajili ya hukumu ambapo Oktoba 1 2021 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo kwa maelezo ya kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.