Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:22 pm

NEWS: SABAYA AFIKISHWA MAHAKAMANI ASOMEWA MASHTAKA LUKUKI

Arusha. Aliyekuwa mkuu wa Wilaya Hai, Lengai Ole Sabaya leo Ijumaa June 4, 2021 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kujibu tuhuma mbali mbali zinazomkabili.

DC huyo wa zamani wa Hai amefikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi akiwa na walinzi wake sita na baada ya kushuka kwenye magari pamoja na wenzake walitakiwa kuchuchumaa kusubiri taratibu nyingine.

Baada ya muda mfupi walichukuliwa na kupelekwa katika chumba maalum wakisubiri kupelekwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Sabaya na wenzake watano ambao ni; Sylivesta Nyegu, Wadson Stanley, Enock Togolan, John Odemba na Daniel Mbura, wamesomewa mashtaka matano katika kesi mbili tofauti mahakamani hapo.

Mashtaka mengine ni; unyang’anyi kwa kutumia silaha, kushiriki vitendo vya rushwa alipokea Sh.90 milioni, kutakatisha fedha na kuongoza magenge ya uhalifu.

Hivi juzi Sabaya alikuwa akihojiwa kwa zaidi ya siku 10 na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma mbalimbali jijini Dar es Salaam na alikuwa chini ya Ulinzi Polisi kwa zaidi ya Wiki 2 akifanyiwa mahojiano.

Kesi ya kwanza, ya Sabaya na wenzake imesikilizwa na Hakimu Martha Mahumbuga na ya pili yenye ya jumla ya mashtaka mawili ya unyang’anyi kwa kutumia silaha na kushambulia aliowanyang’anya imesikilizwa na hakimu mwingine.

Nje ya Mahakama, mkurugenzi msaidizi ofisi ya mashtaka, anayeshughulikia usimamizi wa kesi, Tumain Kweka amesema, uchunguzi kwa baadhi ya makosa, “yanayomkabili Lengai na wenzake, yamefikia tamati ya kuwafikisha mahakamani.”

“Baada ya DPP kujiridhisha, ameamua kuwafikisha mahakamani, alikuwa anatuhumiwa kuendesha magenge ya uhalifu, vitendo vya rushwa, kutakatisha fedha na unyany’anyi wa kutumia silaha,” amesema Kweka.

Amesema, unyany’anyi wa kutumia silaha ni makossa mawili aliyoyatenda kwa watu wawili tofauti.

Mashtaka hayo kwa mujibu wa sheria, hayana dhamana hivyo, Sabaya na wenzake wamepelekwa gerezani hadi tarehe 18 Juni 2021, itakapotajwa tena.

Sabaya amefikishwa mahakamani baada ya kushikiliwa kwa zaidi ya siku kumi na Takukuru, kwa maagizo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.