Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 8:14 pm

NEWS: SABABU YA MAHAKAMA KUHAIRISHA HUKUMU YA SABAYA

Arusha. Hukumu ya kesi ya unyang’anyi kwa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili iliyokuwa itolewe hii leo Octoba 1, 2021 imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2021.

Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Amalia Mushi ambaye ni hakimu katika kesi hiyo amesema bado hukumu hiyo haijakamilika kuandikwa.

Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu na Daniel Mbura, wanakabiliwa na mashtaka matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Inadaiwa katika shtaka la kwanza kuwa Februari 9, 2021 katika Mtaa wa Bondeni, Arusha, washtakiwa hao waliiba Sh2.769 milioni, mali ya mfanyabiashara Mohamed Saad.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, washtakiwa waliwashambulia Numan Jasin, Harijin Saad Harijin, Bakari Msangi, Salim Hassan na Ally Shaban kwa kuwapiga kwa kutumia bunduki, ili kufanikisha wizi huo.

Katika shtaka la pili, Sabaya na wenzake wanadaiwa kuiba Sh390,000 kutoka kwa diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi wakiwa katika Mtaa wa Bondeni.

Walidaiwa kumfunga pingu, kumpiga na kumshambulia huku wakimtishia kwa bunduki kabla ya kufanya tukio hilo.

Hukumu hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 15, 2021 na washtakiwa wote wamerudishwa mahabusu ya gereza la Kisongo.