Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 12:12 pm

NEWS: RUTO AAHIDI KUMPIGIA SIMU RAIS KENYATTA

Rais mteule wa Kenya William Ruto amesema anampango wa kumpigia simu rais anayemaliza muda wake madarakani Uhuru Kenyatta licha ya kuwa hawakuwa kwenye mawasiliano takribani miezi kadhaa.

"Hivi karibuni nitampigia simu rafiki yangu mzuri Rais Uhuru Kenyatta," anasema huku akicheka na kuvutia vicheko kutoka kwa wote wanaotazama.

Inafahamika kuwa Rais Kenyatta na Bw Ruto - ambaye alikuwa naibu wake - walitofautiana miaka kadhaa iliyopita. Bw Kenyatta alimuunga mkono mpinzani wake Raila Odinga.

"Sijazungumza naye [Kenyatta] kwa miezi kadhaa ... najua alifanya kazi kwa bidii kwa njia yake mwenyewe," ambayo ilipokelewa tena kwa kicheko.

"Sichukii kwamba aliamua kuchagua na kumuunga mkono mtu mwingine na kwa hivyo tutabaki marafiki."

Nawanyooshea mkono wa urafiki wapinzani wangu - Ruto

Rais mteule wa Kenya William Ruto anajaribu kukomesha mgawanyiko nchini Kenya na kutengeneza njia ya umoja akisema demokrasia haipaswi kuwa "biashara ya kiharamia".

Alinyoosha mkono wa urafiki kwa wapinzani wake wa kisiasa, akisema waliowapigia kura washindani wake wote wanaitakia Kenya kilicho bora na kwamba amejitolea kutimiza hilo.

"Sisi si maadui, sisi ni Wakenya.

Tuungane kuifanya Kenya kuwa taifa ambalo kila mtu atajivunia kuliita nyumbani kwake."

Pia alisema atatawala kwa ajili ya watu wote, bila kujali "hali zao za kijamii, dini, kabila na jinsia".

Ruto aipongeza tume ya uchaguzi

William Ruto anasifu utendakazi wa tume ya uchaguzi (IEBC) akizungumzia maafisa ambao wamepoteza maisha na wamekuwa wakitishwa “na kila aina ya majaribio ya kupotosha matakwa ya wananchi”.

Lakini pia anawageukia wale waliowasilisha ombi kwa Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya Agosti 9 akisema ni haki yao ya kikatiba.

"Ilikuwa ni halali kabisa kwa walalamishi kwenda mbele ya Mahakama ya Juu ili maswali yao yajibiwe."