Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 7:31 pm

NEWS: RPC ALIYENUSURIKA KUFUTWA KAZI NA RAIS MAGUFULI AHAMISHWA

Dar es salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro amemhamisha aliyekuwa kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Jonathan Shana kwenda kuwa Afisa Mnadhimu shule ya Polisi Moshi.

Katika Taarifa iliyotolewa leo Juni 24, 2020 na Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini SACP David Misime imesema IGP Sirro amefanya uhamisho kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi wa mikoa ili kuongeza ufanisi na tija katika kazi za Polisi.

Pia amemuhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro ACP Salum Hamduni kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha.

IGP Sirro, amemhamisha aliyekuwa Afisa Mnadhimu Bunge, Dodoma ACP Emmanuel Lukula kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro na nafasi yake inachukuliwa na ACP Andrew Satta ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu Makao Makuu ya Polisi Dodoma.

Juzi Juni 22, mwaka huu Rais Magufuli alimuonya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shana Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wateule ambapo alisema kuwa ameamua kumsamehe Kamanda Shana pamoja na Afisa wa TAKUKURU mkoani humo lakini wasifanye makosa.

"IGP na Mkurugenzi wa TAKUKURU mko hapa, mkawaambie watendaji wenu walioko Arusha wafanye kazi nilizowatuma, nao leo nilikuwa niwatoe ambao ni RPC na Mkuu wa TAKUKURU wa Arusha", amesema Rais Magufuli.

"Nimeamua kuwasamehe lakini sijawasamehe moja kwa moja wakifanya kosa lolote wataondoka. Wakafanye kazi nilizowatuma wasifanye kazi wanazojituma wao, haiwezekani watu umewatuma kufanya kazi za serikali wanafanya kazi wanazozijua wao", ameongeza