Home | Terms & Conditions | Help

April 4, 2025, 7:39 am

NEWS: RAIS SAMIA AUNDA KAMATI YA KUSIMAMIA JESHI LA POLISI

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuunda kamati ya wajumbe 12 na sekretarieti ya watu watano kwa ajili ya kufuatilia utendaji kazi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo.

Rais Samia amesema kamati hiyo itakayooongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othumani Chande na makamu wake atakuwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambayo itakuwa ikimshauri njia bora ya kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye matokeo bora kwenye vyombo vya haki jinai.

“Kwa hiyo tutaanza na polisi, wakimaliza wakileta ripoti tutafanya marekebisho, tunakwenda majeshi mengine, tunakwenda magereza, hivyoo mpaka tumalize,” amesema Rais Samia

Rais Samia ametangaza kuunda kamati hiyo Jumatano Juali 20, 2022 mara baada ya kumuapisha Camillus Wambura kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nafasi ambayo ameteuliwa Ramadhan Kingai ambaye awali alikuwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kigoma.

Amesema kwa ufupi serikali inakuja na jicho jingine ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama na kubainisha kamati hiyo itakuwa ikimpelekea mrejesho kila Jeshi linapomalizwa kuchunguzwa na kufanyiwa maboresho.

“Tutakuja na miundo inayofaa sasa hivi ili kuja na jeshi linalofaa na bora kutumikia Watanzania,” amesema Rais Samia

Mbali na IGP Wambura kuapishwa, wengine walioapishwa ni, aliyekuwa IGP Simon Sirro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Luteni Jenerali, Mathew Mkingule kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Dk. Suleiman Haji Suleiman kuwa Balozi.