Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 9:56 am

NEWS: RAIS MWINYI ATUMBUA MAKAMANDA 3 KWA TUHUMA ZA UBADHIRIFU

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Makamanda watatu wa Idara Maalum za SMZ kufuatia kuwepo kwa wafanyakazi hewa na kusababisha upotevu wa fedha za Serikali zaisi ya Tsh. Bilioni 4, ambapo Bilioni 2.2 ni za mishahara hewa na Bilioni 1.8 ni za Posho hewa.

Waliotenguliwa ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Ali Abdallah Ali, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Ali Mtumweni Hamad pamoja na Mkuu wa Kikosi Maalum Cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Comodore Hassan Mussa Mzee.

Akitoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya Habari Ikulu Jijini Zanzibar, leo Aprili 13, Dk. Mwinyi amesema kuwa kufuatia taarifa za uwepo wa wafanyakazi hewa katika Idara Maalum za SMZ, aliunda Kamati ya Uchunguzi kwa kufanya uhakiki wa idadi ya wafanyakazi pamoja na viwango vya mishahara vinavyotolewa kwa vikosi vyote.

Amesema kuwa ripoti ya Kamati ya Uhakiki iliyomfikia ilieleza kwamba kulikuwa na wafanyakazi 381 waliokuwa wakilipwa mishahara bila ya kuwa katika utaratibu unaotakiwa ikiwa na maana kwamba walikuwa watumishi hewa.

Amesema kwamba fedha zilikuwa zikipokelewa na kutumika katika kipindi chote hicho ambapo walikuwa katika vikosi hivyo na kueleza kwamba lililothibitika ni kwamba wakati Kamati imeanza kazi zake baadhi ya vikosi kikiwemo JKU walianza kutengeneza utaratibu wa kurasimisha uwepo wa wafanyakazi hao hewa.

Amesema kwamba waliwahi kukamatwa baadhi ya Maafisa katika nyumba ya mtu binafsi wakiwa wamewafisha sare za Jeshi vijana na kuwapiga picha ili kuthibitisha kwamba wamo katika ajira rasmi.

Rais Mwinyi amesema kwamba imebainika kuwa fedha zilizotumika kwa upotevu ni kiasi cha TZS bilioni 2,235,725,000.00 kutokana na fedha zilizokuwa zikitumika kwa wafanyakazi hewa.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Kamati ilikwenda kuhakiki ulipaji wa posho katika vikosi hivyo ambapo ilibaini wastani wa upotevu wa fedha zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya posho kwa mwezi wa Disemba ni jumla ya TZS milioni 304.1 sawa na wastani wa Sh bilioni 1.8 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba.