Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 4:22 pm

NEWS: RAIS MAGUFULI AWAOMBA WANANCHI KUMPA KURA KUMALIZIA VIPORO VYAKE

Dodoma. Mgombea Urais wa chama cha Mapinduzi CCM Rais John Magufuli amesema amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais kwa mara ya pili ili aweze kumalizia kazi ya kuwatumikia watanzania kwa miaka mingine mitano huku akisema kampeni za chama hicho zitazinduliwa jiji la Dodoma ambapo ndipo Makao Makuu ya Nchi.

Ameyataja mafanikio ambayo serikali yake imeyapata kuwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya zaidi ya 500, Shule za Msingi na Sekondari, umeme kila kijiji sambamba na ujenzi wa barabara za lami ambazo zimerahisisha huduma mbalimbali za kijamii.

Rais Dk John Magufuli ameyasema hayo hii leo Agosti 6, 2020 ofisi za Makao Makuu ya CCM White House jijini Dodoma mara baada ya kurejea kutoka kuchukua fomu hiyo katika ofisi za tume ya uchaguzi nchini iliyopo Njedengwa jijini Dodoma.

k Magufuli ameongozana na mgombea mwenza wake ambaye ni Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai na viongozi wengine wa sekretarieti na Jumuiya za chama hicho.

Rais Magufuli amesema leo Tanzania imefikia uchumi wa kati baada ya kazi kubwa ambayo serikali yake imefanya kwa kuwabana mafisadi na kuzuia mali za Tanzania yakiwemo madini kusafirishwa kiholela kwenda nje ya nchi.

" Wakati tunashughulika na makinikia walisema hatutofanikiwa na tutashtakiwa lakini leo wote tumeona jinsi ambavyo tumefanikiwa na mabilionea wa kitanzania akina Laizer wanachimba na kupata madini tena makubwa ambayo yote yanakuza vipato vyao na uchumi wetu.

Ndugu zangu jinsi ambavyo mimi na Makamu wa Rais Mama Samia tulivyopambana kuboresha umeme vijijini ambapo vijiji 9,402 vimepata umeme ilihali wakati tunaingia mwaka 2015 ni vijiji 3,000 tu vilikua na umeme tukaona tuna kila sababu ya kuomba tena ridhaa ya kuwatumikia nyinyi watanzania," Amesema Dk Magufuli.

Amesema mafanikio yaliyopatikana nchini ni mengi na wala hayatoshi siku moja pekee huku akisema miaka mitano mingine itakua ni ya kazi zaidi bila kulala lengo likiwa kukuza zaidi uchumi wa Tanzania na kuwasogezea wananchi huduma zaidi.

" Wanasema nitapigiwa kura na Ndege, Madaraja na Vituo vya afya, mimi nasema asante sana maana wananipigia kampeni, tumenunua ndege 11 tena kwa hela zetu cash hatujakopa na Leo tunaona matunda yake, tumejenga flyover ambazo tulizoea kuziona kwenye Runinga sasa zipo kwetu na tunazitumia.

Treni za Umeme siyo ndoto tena ujenzi wa Reli ya Kisasa unakaribia kukamilika ili treni hizo zipite, ndugu zangu kwa hayo yote nikasema mtu pekee wa kumalizia kazi iliyobaki ni mimi na Mama Samia na chama chetu cha Mapinduzi, " Amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli amewataka wanachama wa chama hicho kutobweteka kujiona tayari CCM imeshashinda badala yake wazidi kupiga kazi ili kura walizonazo zisipungue.

Awali akimkaribisha Dk Magufuli, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema wako tayari kuwakabili wapinzania na kwamba wanaenda kwenye uchaguzi huu wakiwa wenye kujiamini kutokana na mafanikio ambayo yamepatikana kupitia kwake Rais Magufuli na serikali yake.

Amesema wao kama viongozi watafanya kampeni za kistarabu na kuwataka wanachama wa CCM kutolala badala yake wapige kampeni za Mtaa kwa Mtaa, Nyumba kwa Nyumba na kitanda kwa kitanda.

" Ndugu mgombea wetu utendaji wako mahiri wa kazi ndio unaotupa imani ya kwamba tutaibuka washindi katika uchaguzi huu, Jumuiya zetu tumeshazigaia majukumu na zitafanya kazi mchana na usiku kuhakikisha ushindi unapatikana wa kishindo," Amesema Dk Bashiru.