Home | Terms & Conditions | Help

April 3, 2025, 12:04 pm

NEWS: OFISI YA RAIS UTUMISHI YATOA MAAGIZO KWA WAAJIRI WOTE NCHINI.

DODOMA: Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Xavier Daudi amewataka waajiri wote nchini kuwaruhusu Wakuu wa idara za utawala na usimamizi wa rasilimali watu katika Wizara, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, idara zinazojitegemea, taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali kuwaruhusu kuhudhuria kikao kazi cha mwaka cha Wakuu hao.


Ameitoa maagizo hayo Desemba 12,2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Wizara hiyo kuhusu kuanza kwa kikao hicho mnamo Desemba 17 hadi 19 mwaka huu Jijini Dodoma.

Daudi amesema kutokana na umuhimu wa kikao kazi hicho amewataka Waajiri wote nchini kuwaruhusu Wakuu hao wa Idara kushiriki kikamilifu katika kikao kazi hicho ili kujifunza mbinu mbalimbali za kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza malalamiko.


"Nitoe rai kwa wahusika wote wa kikao hicho cha Desember 17 hadi 19 wafike katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo katika Mji wa Serikali Mtumba tarehe 16 Disemba, 2024 kuanzia saa 10:00 Jioni ili kuchukua vitambulisho na makabrasha kabla ya kuanza kikao , "amesema

Ametaja malengo ya kikao kazi hicho kuwa ni kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na ukumbushana masuala mbalimbali yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali ya e-Watumishi, e-Uhamisho, e-Utendaji, e-Mrejesho, HR Assessment.

Lengo lingine ni kupeana maelekezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika utumishi umma kwa kuzingatia Shabaha na vipaumbele vya Taifa.

Mbali na hayo pia amewataka Wakuu wote Kujisajili kwenye mfumo wa https://tsms.gov.go.tz ili kushiriki kikao hicho na kwamba mwisho wa kujisajili ni tarehe 13 Desemba, 2024.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma Felister Shuli amesema Rasilimaliwatu ni nguzo ya Uendelezaji wa rasilimali zingine hivyo ni muhimu kujengewa uelewa.

Amesisitiza kuwa ufanisi wa Taasisi hutegemea uwezo na maarifa ya wafanyakazi wake na kuongeza kuwa uwepo wa mifumo bora ya usimamizi wa rasilimaliwatu kutasaidia kuboresha utendaji kazi, kupunguza urasimu, na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine mengi,kikao kazi hicho kitaongozwa na Kaulimbiu isemayo "Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala ya Kidijitali iliyoboreshwa” na Mgeni Rasmi wakati wa Ufunguzi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Mwishoo