Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:45 pm

NEWS: NJIA MBADALA ZITUMIKE KUTAMBUA IDADI KAMILI YA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM.

DODOMA: Serikali kwa kushirikiana na wananchi wametakiwa kutumia njia mbadala ili kuweza kutambua idadi kamili ya watoto wenye mahitaji maalum lengo kuwaandikisha shule za watoto wenye mahitaji maalumu kama vile vipofu,walemavu wa viungo , viziwi na bubu.

Kwa mujibu wa Ripoti iliyotolewa na Wanajamii wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma baada ya uchambuzi uliofanywa na shirikia lisilo la Kiserikali ACTION AID Tanzania imesema ili kufanikisha malengo ya kila mtoto aliyefikisha miaka ya kuandikishwa shule awe shuleni bila kujali hali yake basi Serikali inawajibu kuhakikisha shule zilizotengwa ziwe na miundombinu wezeshi na uwepo wa walimu wenye mafunzo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

''Serikali itoe ruzuku kwa kila shule kulingana na idadi ya wanafunzi na pia watoto wenye ulemavu waongezewe kiasi cha ruzuku ili kukidhi mahitaji yao, pia serikali itoe au kupunguza kodi kwenye vifaa vinavyotumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalum mfano bei ya viti mwendo huuzwa kwa bei sh. 250,000 hiki ni kiasi kikubwa familia nyingi zinashindwa kununua,'' alisema Ester Maile. msoma taarifa

Maile alisema katika uchambuzi huo idadi ya watoto wenye mahitaji maalum walioandikishwa shule ni 81 , ambao hawajaandikishwa 80 hii hatari kwa taifa lijalo kwani kutakuwa na ongezeko kubwa la watoto ambao watakuwa tegemezi kwa taifa na watakaoshindwa kuajiriwa na kuongezea idadi ya watoto wa mitaani.

Mbali na hayo Maile alisema katika halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kati ya shule 20 zilizotembelewa zinauhitaji wa madarasa 374 sawa na asilimia 49.73 ya uhaba unapelekea kusomea chini ya miti mfano Shule ya msingi Mapinduzi.

''Serikali pamoja na wadau wa elimu kujenga miundombinu ambayo ni rafiki kwa wanafunzi wote mfano baadhi ya madarasa hayana ngazi mserereko kwa ajili ya watoto wanaotumia viti mwendo,'' alifafanua Maile.

Alisema Umbali wa shule kufikiwa kwa wananfunzi wote bado ni changamoto kwani baadhi ya shule zipo umbali mrefu kutoka kwenye makazi ya watu,hivyo hupelekea baadhi ya watoto kukosa vipindi vya mchana msimu wa mvua,''mfano shule ya Mloda kwa watoto wanaotoka kitongoji cha Maumi wanafunzi hutembea umbali mrefu takribani kilomenta 15 (umbali wa kwenda na kurudi kila siku) nakushauri ujenzi wa shule uende sawia na jiografia ya maeneo na makazi ya watu na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa elimu.

Pamoja na hayo aliongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyokuna uhaba wa mkubwa wa matundu ya vyoo ukilinganisha na namba ya matundu yaliyopo mfano uhitaji wa matundu ya vyoo kwa shule 20 zilizotembelewa ni matundu 653 wakati yaliyopo ni matundu 205 ikiwa upungufu ni 448.

''Kwa shule 20 zilizofanyiwa uchambuzi katika zoezi hili imefahamika kuwa kuna uhitaji wa madawati 6470 lakini yaliyopo ni 3328 huku upungufu ni madawati 3142 sawa na 48.56%.

Nao baadhi ya Madiwani akiwemo Diwani wa kata ya Chilonwa Alfa Mtura na Diwani kata ya Iringa Mvumi Robert Chikole walikiri kuwepo kwa changamoto hizo katika elimu na kudai elimu inatolewa katika jamii na mikakati imewekwa kwa wananchi kuanzisha ujenzi wa maboma ya ujenzi wa shule na Serikali kutoa fedha kwaajili ya umaliziaji.

Naye afisa Mipango wa Wilaya ya Chamwino John Masero alisema kuwa pamoja na Serikali kuhimiza wananchi kujenga maboma ili itoe fedha kwaajili ya kuyakamilisha, katika Wilaya hiyo imekuwa ni changamoto kutokana na umaskini wa watu wake.

Majumuisho ya Uchambuzi yaliyofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali la ACTIONAID TANZANIA kwa kushirikiana na AFNET yalifanyika katika kata sita za Wilaya ya Chamwimo ambazo ni kata ya Msanga, Chilonwa,Chamwino,Buigiri,Mlowa, A na B, na Makang'wa.