Home | Terms & Conditions | Help

April 5, 2025, 4:56 pm

NEWS: NDUGAI AWATAKA VIONGOZI WA KIKE KUACHA KUVIMBA

Dodoma. Spika wa bunge wa Tanzania Job Ndugai amewataka viongozi wanawake wenye mamlaka ya Serekali kuacha tabia ya kuvimba na kushuritisha watu wanapopewa mamlaka kwa kuwaweka watu ndani hovyo, kwani kufanya hivyo kunawaondolea sifa ya kuwa viongozi.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Novemba 10, 2021 katika ukumbi wa Pius Msekwa bungeni alipokuwa akizindua mafunzo ya uongozi kwa wabunge wanawake.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika uongozi.

Spika amesema Taifa linaloongozwa na mwanamke linakuwa tulivu , amani na salama.

"Lakini kauli za baadhi zinaharibu taswira nzima, wengine mavazi yenu yanakuwa ya hovyo, ukipewa cheo kazi yako inakuwa ni kufoka na kuweka watu ndani jambo linaloharibu taswira ya viongozi wakuu wa nchi," amesema Ndugai.

Spika Ndugai amewaagiza wabunge wanawake kujifunza kwa bidii mafunzo hayo kwani ushahidi unaonyesha waliojifunza walibadilika na kuwa viongozi mahiri.