- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: NDUGAI ATAHADHARISHA NCHI KUPIGWA MNADA
Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ametahadharisha Viongozi na Umma wa Watanzania kuwa kuna siku nchi itapigwa MNADA ikiwa itaendeleza tabia ya kukopa kopa na kuwa na madeni makubwa makubwa ambayo hayaeleweki.
Ndugai amesema kuwa ni vyema watanzania wenyewe wabanane kupitia tozo za miamala ya simu ili fedha zinazopatikana zinakwenda moja kwa moja kujenga madarasa, vituo vya Afya na mambo mengine ya kimaendeleo nchini.
Hayo ameyasema Jana Desemba 28, 2021 katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma.
“Juzi mama(Rais Samia) ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi),” alisema Spika Ndugai.
Spika alisema “Tutembeze bakuli ndio heshima, tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku, Ndugai amesema huku akitetea tozo kwamba; “Tukasema pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.
Ndugai aliendelea kufafanua juu ya yeye kupinga swala zima la nchi Kukopa madeni makubwa kutokana na Deni la taifa kufikia tsh. Trilioni 70, kitu ambacho Spika Ndugai alisema hii haiko sawa kwa Afya ya Uchumi wa Tanzania.
“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alihoji Ndugai kwenye mkutano huo wa kimila wa kabila la Wagogo" alisema Spika Ndugai.
Kauli ya Rais Samia kukinzana na Kauli ya Spika.
Hata hivyo, kwa upande mwingine, kauli hiyo ya Spika Ndugai imeonekana kutofautiana vikali na mtazamo wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani Juu ya kufanya maaamuzi ya kukopa kwenye miradi mikubwa ya kimaendeleo.
Wakati Rais Samia akizungumza leo Desemba 28 katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa SGR uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam, amesema Serikali itaendelea kukopa ili kukamilisha ujenzi wa reli hiyo.
Mkataba huo wa leo ulilenga kukamilisha kipande cha tatu kutoka Makutupora hadi Tabora chenye urefu wa kilometa 368, kitakachogharimu dola za kimarekani dola 1.908 bilioni sawa Sh4.41 trilioni kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Yapi Merkez kutoka Uturuki.
Rais Samia amesema "Kama nilivyosema uwekezaji mpaka sasa ni Sh14.7 trilioni hivyo tusipoendeleza ujenzi huu tukakamilisha, fedha tulizolaza pale chini zitakuwa hazina maana. Kwahiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote tutakopa… tutaangalia njia rahisi, zitakazotufaa za kukopa
“Kwani fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani ni lazima tutakopa ili kukamilisha mradi huu. Ni lazima tukope twende tumalize huu mrad,” amesema Rais Samia.
Amesema Mradi wa SGR ulianza kutekelezwa kwa mujibu wa ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ulianza mwaka 2017 na umegawanyika katika vipande vitano ukipita katika mikoa tisa.
Amesema kwasasa ujenzi huo unaendelea katika vipande vitatu cha Dar es Salaam- Morogoro (asilimia 95), Morogoro- Makutupora (asilimia 77) na Mwanza-Isaka (asilimia 4) ambapo ni jumla ya kilometa 1063 za njia kuu za reli pamoja na njia za kupishana.
Rais amesema “Hii ni kazi kubwa yenye kuhitaji uthubutu mkubwa wa serikali na wananchi wake. Hii inafanya uwekezaji wa ujenzi wa vipande vinne kati ya vitano vinavyoendelea kufikia kiasi cha sh 14.7 trilioni ukijumlisha na kodi,”
UCHAMBUZI WA KIMTANZAMO.
Sasa kauli hizo Mbili za viongozi wakuu wa nchi zinaleta ukakasi katika kuendesha gurudumu la maendeleo nchini na kuzua taharuki kwa Watanzania juu ya kauli ipi ishikwe au ipi iachwe na ukizingatia Spika wa Bunge ndio anayepitisha Bajeti ya nchi, kutunga miswada mbalimbali ya nchi na kuisimamia Serekali huku na Rais kama kiongozi mkuu wa Nchi mwenyekubeba Dira na maono ya nchi, mwenye kuandaa bajeti na kupanga mambo mabli mbali ya nchi .
Kumbuka Serekali inayoongoza nchi ni Serekali ya Chama cha mapinduzi ambapo Rais Samia anatoka kwenye chama hicho na ni Mwenyekikiti wa Chama hicho, huku Spika wa Bunge Job Ndugai naye ni mwanachama wa chama hicho na ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chama.
Tulitarajia kwamba kwakuwa viongozi wote hawa wawili wanatoka chama kimoja basi wataongea lugha moja kwasababu Serekali wanayoiongoza inatokana na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ambayo wote wawili waliinadi na kupigiwa kura na watanzania kwa kutumia Ilani hiyo.
Imeandikwa na Deyssa Issa.
Na Kuhaririwa na Merry Mgawe
Muakilishi Publisher Desemba 28, 2021