- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MUUNGANO WA WAGOMBEA TISA WA URAIS WAJA KENYA
KENYA: WATU tisa ambao wamejitokeza kutaka kuwania urais mwaka huu 2022 nchini Kenya, wanapanga kumteua mmoja wao kumenyana na wagombea wakubwa ambao ni Raila Odinga (Azimio) na William Ruto (Kenya Kwanza) Agosti 9.
Wakizungumza na wanahabari Alhamisi jijini Nairobi, wawaniaji hao walisema kuwa wataungana na kuunda muungano wa Eagles National Alliance.
Wakiongozwa na Walter Mong’are ‘Nyambane’ wa chama cha Umoja Summit, walisema kuwa nia yao ni kumteua kiongozi atakayetetea maslahi ya wananchi wa kawaida bila ubaguzi.
Bw Mong’are alisema kuwa atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya urais kupitia muungano huo, ataungwa mkono na makanisa nchini.
“Tumechoka kuwachagua viongozi ambao nia yao ni kuendelea kufilisisha uchumi wa nchi. Tunataka mabadiliko. Kwa hivyo tumekuja pamoja kama wawaniaji wa urais, ili tuweze kuuunganisha nguvu na uwezo wetu. Tunataka tuunde serikali yenye sura mpya,” akasema Bw Mong’are.
Kulingana na mpango wa wanasiasa hao ambao wamejitokeza kuonyesha azma ya kutaka kuingia ikulu, hivi karibuni watamtangaza hadharani atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya urais wa muungano wao.
“Katika siku chache zijazo, tutamtangaza rasmi mgombea wetu wa urais. Hata sisi tuna uwezo wa kuiongoza nchi hii. Baadhi yetu tuna ajenda ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi wa nchi,” akaongeza Bw Mong’are.
Viongozi hao wanawaomba Wakenya wasitawaliwe na kasumba kuwa farasi ni wawili katika uchaguzi wa Agosti.
“Kila mmoja ana uwezo wa kuiongoza nchi hii. Wakenya wajiepushe na kasumba kuwa farasi ni wawili. Hata sisi tuna uwezo wa kutawala Kenya,” akasema Bw Mong’are.
Kura za maoni za mashirika kama Infotrak na Trends and Insights for Africa (TIFA), zimeonyesha kuwa Bw Odinga na Dkt Ruto wako kifua mbele kwenye kinyang’anyiro hicho.
Kulingana na wachanganuzi wa siasa, itakuwa vigumu wawaniaji wadogo wadogo wa urais kupenya katika ngome za wawili hao, kwa kuwa umaarufu wao umeenea sana.
Mbali na Bw Mong’are, anayetaka urais kupitia chama cha Agano, Bw David Mwaure, alisema kuwa muungano wao utafuata mwongozo wa kidini.
Maadili na mafunzo ya kiroho vitatumika wakati wa uteuzi, ili mchujo wa kumteua mmoja wao uwe wa huru na haki.
Alisema anayetaka kuwa rais hafai kuwahadaa wananchi kwa kuwapa pesa za hongo, ambazo hazina manufaa ya kudumu.
“Hakuna haja wananchi waendelee kuteseka mikononi mwa viongozi ambao wamekuwa serikalini miaka nenda miaka rudi. Tunaamini kuwa yote yanawezekana, ikiwa tutamchagua kiongozi anayefaa,” akasema Bw Mwaure.
Wengine ni Reuben Kigame, Duncan Oduor Otieno, Dkt Japheth Kaluyu, Kasisi Joe Kamau, George Munyottah, na Dkt Justus Juma.
Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanywa Agosti 9 unazidi kuibua joto la kisiasa nchini huku ikibainika wazi kuwa farasi wawili watakuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto.