Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 7:30 pm

NEWS: MTATURU AZIDI KUNG'ARA JIMBONI, KELELE ZAKE BUNGENI ZAZAA MATUNDA KIJIJI CHA MAHAMBE,

SINGIDA; “Maisha yetu kila siku ilikuwa ni kuamka asubuhi sana kwenda kutafuta maji,wakati mwingine tunalazimika kutumia muda wa kufanya shughuli zetu za kiuchumi kusaka maji hali iliyoturudisha nyuma kimaisha,lakini tunamshukuru Mbunge wetu Miraji Mtaturu ametusaidia kuondokana na adha hii,”.



Ni maneno ya mkazi wa Kijiji cha Mahambe Sophia Hamisi,maneno hayo yanawasilisha shukrani kutoka kwenye kinywa chake yeye kwa niaba ya wanakijiji wenzake ambao wameteseka kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa maji kijijini hapo.



Sophia anasema,“Leo tunasherehekea kupata maji,tumewahi kuwa na wabunge kwa awamu mbili wanaotoka katika kijiji hiki lakini hatujawahi kuona manufaa,sasa mbunge wetu Mtaturu ameweza kuleta maji na kutupunguzia kero ya maji tuliyokuwa tunaipata,wanakijiji tuna neemeka na maji safi na salama tunayopata,sasa hatuwazi maji tena bali tunatumia muda wetu kufanya shughuli za kuzalisha kipato,”anasema Sophia.



Haji Njau ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahambe Kati ambaye anamshukuru Mbunge kwa kuwakilisha vizuri matatizo yao na serikali ikasikia na hatimaye maji sasa sio shida kwao.



“Mtaturu amekuwa mfano wa kuigwa kati ya wabunge waliowahi kuongoza jimbo hili la Singida Mashariki,aliahidi kutuletea maji na ametekeleza kutuletea mradi endelevu na sasa adha ya maji imeisha ,jambo hili liwe mfano kwa wabunge wengine pia,”anasema Njau.



Kupatikana kwa huduma hiyo ya maji kumefuatia baada mbunge Mtaturu kutoa Sh Milioni 9.7 kutoka kwenye mfuko wa Jimbo ili kuwapatia miundombinu ya maji kutoka kwenye kisima kilichochimbwa na mfadhili tangu mwaka 2013.



Aidha,Mbunge Mtaturu ameweka Tanki la Lita 10,000, mabomba yenye urefu wa mita 770 na vituo viwili vya kuchotea Maji ambapo wananchi nao walitoa nguvu kazi kwa kushiriki uchimbaji wa Mtaro wa kusambaza maji.



Mara kadhaa Mbunge Mtaturu awapo bungeni pamoja na Mambo mengine kilio chake kikubwa kilikuwa kwenye sekta ya maji,na swali lake la kwanza alilouliza katika kipindi chake Cha kwanza Cha ubunge wake lilihusu maji.



Aidha,katika mchango wake kwenye Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka 2021/2022 alitaja Mambo manne ya kuzingatiwa Ili kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji katika wilaya ya Ikungi akiwemo kuhakikisha vijiji kumi vinapata chanzo cha maji cha uhakika.



Vijiji hivyo ni Ntuntu,Tharu,Mbogho,Mwau,Mahambe,Choda,Manjaru,Tumaini,Matongo na Unyakhanya.



“Nikupongeze Waziri na timu yako kwa kazi nzuri mnayoifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata maji,na Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM katika ukurasa wa saba Ibara 9 D kifungu cha kwanza imeeleza wazi katika miaka mitano kuwa itaongeza nguvu katika upatikanaji wa maji,



“Hivyo katika hili kasi inatakiwa iendelee kuongezeka katika kuwekeza zaidi, najua kazi imefanyika na mimi nina ushahidi katika jimbo langu au Wilaya ya Ikungi tumepata bilioni 3.7 kwa mwaka uliopita,safari hii naona wametubana sana kwa wilaya nzima tumepata Bilioni 1.7 ,maana yake kwa hali ya maji tuliyonayo katika wilaya yetu bado tupo chini sana nina amini kunahitajika juhudi kubwa kuongeza fedha kwa ajili ya kuwekeza zaidi,”alisisitiza Mtaturu wakati anachangia hotuba hiyo.



Jambo la pili alilolitaja ni kuhusu usimamizi wa miradi hiyo ili fedha zilizowekezwa ziweze kuleta tija kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.



Jambo la tatu ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Ikungi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha katika utekelezaji wa miradi ya maji.



Na Jambo la nne Mtaturu alilolitaja ni kuongeza uwezo wa uchimbaji wa mabwawa ya maji ili kupunguza tatizo la maji katika maeneo yao hasa kwenye eneo la kunywesha mifugo na hata kufua.



Wakati akilihutubia bunge, Rais Samia Suluhu Hassan alisema anachukizwa kuona mwanamke anabeba ndoo kichwani hivyo aliahidi kutafuta fedha na kupeleka kwenye miradi ya maji ili aone akina mama wanachota maji nyumbani na katika hilo alisema watu wakipenda wamuite mama maji.



Rais Samia (Mama Maji),ameupiga mwingi katika kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo,na Wakazi wa Mahambe wanasema Kazi Iendelee