- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MTATURU APAZA SAUTI BANDO YA SIMU
DODOMA: Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishauri Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),kuwasimamia watoa huduma wa simu ili kuondoa malalamiko yaliyopo kwa wananchi kuhusu kifurushi cha mawasiliano kuisha kabla ya muda wake.
Aidha,ameiomba serikali kuangalia gharama zinazotozwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),hususan kwa safari ya kutoka Dodoma kwenda Dar es salaam ambazo ni kubwa.
Mtaturu ametoa ushauri huo Februari 15,2022 Jijini Dodoma wakati akichangia taarifa ya kamati ya bunge Miungombinu ambapo amesema kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu vifurushi vya simu ambayo wanayapokea kutoka kwa wananchi.
“Malalamiko haya tunayapokea kuhusiana na vifurushi vya simu vya wiki moja,unakuta mtu amejiunga na kifurushi,wiki ikiisha hajamaliza zile fedha zinaondoka wakati alililipia mwenyewe,wananchi wanalalamika tunaiomba serikali iwasaidie wananchi waweze kupata haki yao wanapoweka bundle kwenye simu zao,”alisema.
Amesema hilo limekuwa ni tatizo na majibu yamekuwa hakuna na hata watoa huduma kwa mteja wakipigiwa simu wanakuwa hawana majibu ya moja kwa moja katika eneo hilo.
“Tunaomba serikali ilifanyie kazi ili kuwapa haki wateja ambao ni wananchi wetu huko vijijini,tumezungumza kwenye kamati na nimeona niliseme hapa ili wananchi wafahamu,”alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu ATCL Mtaturu amesema kuna maeneo mawili ambayo ni changamoto ikiwemo suala la bei za tiketi ya ndege.
“ATCL wanafanya kazi nzuri,tumewanunulia ndege zakutosha na zinazunguka nchini,lakini kuna maeneo mawili ambayo ni changamoto kubwa la kwanza bei za tiketi ya ndege, leo hii ukiangalia bei kutoka Dar es salaam hadi Dodoma gharama inafikia laki nne hadi laki saba ambayo ni kama unaenda Dubai wakati upo Tanzania,”aliongeza.
KUHUSU MIUNDOMBINU YA BARABARA .
Mtaturu amesema kumekuwa na kikwazo cha kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali (GN)ambapo wahusika ni wizara za fedha na hata kama fedha zimetengwa kwa ajili ya kutoa GN ili kuruhusu barabara kujengwa imekuwa ni tatizo.
“Eneo hili niiombe sana serikali ikae pamoja,haiwezekani wizara ya ujenzi inalalamikia wizara ya fedha ,haiwezekani wizara ya mawasiliano inalalamikia wizara ya fedha, haiwezekani kwa kuwa serikali ni moja,kupitia kamati tumejadili na tunaendelea kuishauri serikali GN itoke mapema ili kuruhusu barabara hii ijengwe kwa wakati na hivyo kuharakisha maendeleo,”alisema.
Amempongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya ya kujenga nchi.
“Tumepitia taarifa zote zinazoeleza utendaji kwa mwaka mzima tumeona fedha zimeletwa za kutekeleza miradi mbalimbali katika majimbo yetu na kwenye nchi yetu,na kama mnavyojua barabara zinazounganisha mikoa na mikoa zinasaidia katika uchumi wa nchi yetu,”alibainisha.
Ametolea mfano barabara ya Singida – Mtoro - Kiblashi Tanga na barabara ya Mkiwa kupitia Itigi hadi Makongorosi Mbeya na barabara nyingine zinazotoka Singida - Hydom ni barabara ambazo ni muhimu katika uchumi wa nchi.
“Mpaka hivi ninavyoongea bado barabara hizo hazina wakandarasi tusitegemee katika muda wa mwaka wa fedha uliobaki tukianza leo kutangaza kama barabara hizo zitakamilika, niombe serikali iweze kuhakikisha kwamba barabara hizo zinaanza kujengwa ili kufikia malengo yaliyopangwa katika bajeti tunayoimalizia ,
Amewapongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwa mfano katika kurekebisha barabara ,kujenga barabara mpya na kuwasimamia wakandarasi .