Home | Terms & Conditions | Help

November 21, 2024, 5:34 pm

NEWS: MSD WATAFUNA MABILIONI YA PESA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya maafisa ununuzi wa umma kukubali zabuni za watoa huduma zenye bei ya juu kuliko bei halisi za soko na kuahidi kuwa ataanza na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) kulishughulikia suala hilo.


Waziri Mkuu ametoa onyo hilo jana Alhamisi, Mei 5, 2022) wakati akizungumza na wataalamu wa ununuzi na ugavi pamoja na wasimamizi kwenye uzinduzi wa Wiki ya Ununuzi wa Umma iliyoanza leo katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha AICC, jijini Arusha.

"Pamoja na uwepo wa taasisi zinazosimamia manunuzi yanayofanywa katika ofisi zetu, bado wasimamizi wa manunuzi hawajaona huruma kwa walipakodi wetu kwa kuendelea kufanya manunuzi kwa gharama kubwa," amesema Waziri Mkuu na kutolea mfano manunuzi yaliyofanywa na maafisa manunuzi wa MSD ambao wamenunua vifaa kwa gharama kubwa tofauti na bei halisi ya soko.

Amesema kupitia fedha ya UVIKO-19 ambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alienda kukopa nje, ilitolewa fedha kupitia Wizara ya Afya ili zinununue vifaa vya tiba kwa ajili ya hospitali za mikoa, za rufaa, vituo vya afya na zahanati kwa nia ya kuwapunguzia mzigo Watanzania wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za tiba.

“MSD ilipata mgao wa fedha na ilipaswa kununua baadhi ya vifaa na nataka nitoe mfano huu: Walipaswa kununua kipimo cha sukari (blood glucose test) kwa sh. 150.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 300.00. Walipaswa kununua kifaa cha kupima mkojo (urinalysis) kwa sh. 200.00 lakini wao walikinunua kwa sh. 780.00”



“Walitakiwa kununua kipimo kidogo cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 2,100 lakini wao walikinunua kwa sh. 4,500; pia walitakiwa kununua kipimo kikubwa cha hematolojia ya mwili (Full Blood Picture 3 part) kwa sh. 3,800 lakini wao walikinunua kwa sh. 6,300; na walitakiwa kununua kipimo cha kuangalia ufanyaji kazi wa figo na ini (Renal and Liver Function Test) kwa sh. 6,000 lakini wao walikinunua kwa sh. 40,000.”