Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 5:11 pm

NEWS: MSAJILI AVIONYA VYAMA VYA ACT NA CHADEMA KUUNGANA

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Sisty Nyahoza, amevitahadharisha vyama vya siasa nchini vinavyotaka kuungana siku ya Oktoba 3 mwaka huu, kuacha mara moja mpango huo kwani wanakiuka utaratibu wa sheria na kwamba walianza vizuri hivyo ni vyema kila mmoja akaendelea kunadi sera zake.

Kauli hiyo ya Msajili inakuja baaada ya Kiongozi mkuu wa chama cha ACT wazalendo Zitto kabwe kutoa taarifa kuwa chama chao kitatoa msimamo wa iwapo vitaunganisha nguvu na chama kikuu cha upinzani nchini Chadema.

Nyahoza ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba Mosi, 2020, kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio na kuongeza kuwa hata hivyo tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekwishaviandikia barua vyama hivyo kwa kuwa ni masuala ya kiofisi huwa hawaziweki barua hizo hadharani.

"Kwanza tunaawaasa hao wanaotaka kufanya hivyo tarehe 3 sisi kama walezi wa vyama vya siasa kwa sababu wanakiuka sheria, walianza vizuri hivyo kila mmoja aendelee kunadi sera yake na wagombea wao wa urais", alisema Nyahoza.

Msajili amekumbusha kuwa sheria ya vyama vya siasa inawekwa kwa maslahi ya wanachama na wananchi na unapotaka kushirikiana hutakiwi kufanya kitendo chochote kinachohadaa wananchi kwa hiyo ni kosa kufanya hivyo ghafla wakati wa uchaguzi.

“Ukiunganisha nguvu na chama kingine wakati mmeshakubaliana na wananchi kwamba mtatekeleza sera gani ni kuwahadaa, sisi tulishawasiliana nao na tukawaambia waache," alisema Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini Nyahoza.