Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 2:51 pm

NEWS: MPANGO ATAKA KUPITIWA UPYA MRADI WA BWAWA LA MWALIM NYERERE

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ameagiza Wizara ya Nishati, Shirika la Tanesco pamoja na Mkandarasi kupitia upya mpango kazi wa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kufua umeme la Julius Nyerere pamoja na kuongeza vitendea kazi na muda wa kufanya kazi ili kuepusha kucheleweshwa kwa mradi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere.

Mpango amesema ni muhimu wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuimarisha usimamizi, kuongeza wataalam sehemu zenye upungufu pamoja na kuongeza umeme utakaoendesha vema mitambo ya mkandarasi wakati huu wa ujenzi wa mradi.

Mpango amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa wakati ambapo mpaka sasa jumla ya Sh Trilioni 2.8 zimelipwa kulingana na mkataba.

Aidha, amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kampuni ya kitanzania ya TECU kwa kuendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa watanzania pamoja na kutumia malighafi za Tanzania katika ujenzi wa mradi huo.

Katika hatua nyingine ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kulinda mradi huo wakati wote ili kuepusha hujuma zinazoweza kujitokeza wakati na baada ya ujenzi.

Pia amewaagiza viongozi wa mikoa kuchukua hatua kali kudhibiti idadi ya mifugo iliopo na inayoingizwa katika Bonde la mto Rufiji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa bonde hilo kwa manufaa ya mradi.