- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MFUNGWA ALIYEACHILIWA KWA MSAMAHA WA RAIS AMUUA MAMA YAKE
Kenya. Mwanaume mmoja nchini Kenya aliyeachiliwa huru kwa msamaha wa Rais Kenyatta wiki mbili zilizopita, sasa anasakwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi kwa madai ya kugombania Shamba.
Maafisa wa polisi katika Kaunti ya Kirinyaga wanamsaka jamaa huyo anayesemekana kumuua mamake mzazi kwa kumkatakata, kutokana na mzozo wa ugawaji wa shamba.
Mwanaume huyo aliyekuwa miongoni mwa wafungwa 3,908 walioachiliwa kwa msamaha wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye Sherehe ya Madaraka day anashukiwa kumuuwa mamake Grace Muthoni Ndambiri, bafuni nyumbani kwake kijijini Njoga siku ya Jumapili kisha kutoroka.
Majirani waliofika katika eneo la tukio walimkuta mama huyo akiwa ameuawa na kupiga ripoti kwa polisi mara moja.
Bosi wa polisi katika Kaunti ndogo ya Mwea Mashariki, Daniel Kitavi alisema kuwa maafisa wa polisi waliupata mwili wa mwathiriwa na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Kibugi.
“Mwathiriwa alikatwakatwa kwenye kichwa. Maafisa waliupata mwili wake huku damu imetapakaa kila mahali” akasema Bw Kitavi.
Kabla ya mauaji, mshukiwa huyo alikuwa akizozana na mama yake kuhusu ugawaji wa shamba.
“Baada ya kusamehewa na Rais Kenyatta Sikukuu ya Madaraka na kurudi nyumbani, wawili hao wamekuwa wakizozania ugawaji wa shamba. Mshukiwa amekuwa akimtaka mwathiriwa kumgawia kipande cha shamba. Huenda alimuuwa baada ya mamake kukataa kutimiza matakwa yake,” akasema Bw Kitavi.
Hata hivyo, Bw Kitavi alisema kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na kisa hicho na pia kujua kwa nini mshukiwa alimuuwa mamake mzazi.
Alisema kuwa maafisa wa polisi na wakazi wa kijiji hicho wamekuwa wakimsaka mshukiwa huyo pindi tu walipoupata mwili wa mamake na kugundua ametoroka.
Bw Kitavi alisema mwathiriwa amekuwa akiishi na mwana wake baada ya mumewe kuugua na kufariki.
“Watoto wake wengine wameajiriwa. Mwathiriwa alikuwa akiishi na mwana wake huyo aliyegeuka mhalifu ambaye mwishowe alimtendea unyama huo,” akasema Bw Kitavi.
Kadhalika, alisema kuwa mshukiwa atakapopatikana atashtakiwa kwa mauaji.
Hata hivyo, wakazi wa kijiji hicho wameelezea hofu yao baada ya mauaji hayo, jambo linalowafanya wengi kuishi kwa uoga.
“Kilichotokea hapa ni cha kushangaza sana. Hatujawahi kuona tukio kama hili,” akasema Joyce Wambui, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.