- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: MEMBE ARUDISHA KADI YA CCM
Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje ya nchi wa Tanzania, na mwanachama mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bernard Membe, leo Julai 6, 2020 ameamua kurejesha kadi ya uanachama wa Chama hicho aliyoipata kwa zaidi ya miongo 3 iliyopita.
Membe amerejesha kadi hiyo akiwa amesindikizwa na mkewe, pia ameandika barua kwenda kwa viongozi wa chama hicho kukishukuru chama hicho kwa wema wote waliomtendea.
Kiongozi huyo wa zamani amerudisha kadi ya uanachama ingawa Chama cha Mapinduzi kinadai kilishamfukuza uanachama .
Membe alidai kuwa taratibu za kichama hazikufuatwa, na hivyo bado alikuwa mwanachama halali wa CCM.
Hii leo Membe hajasema anaelekea chama gani cha siasa japo wiki iliyopita aliiambia BBC kuwa endapo upinzani nchini humo utaungana na kumwomba ajiunge atafanya hivyo.
Membe pia anatarajiwa kugombea urais mwezi Oktoba.
Wiki iliyopita, Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe alimualika Membe ajiunge na upinzani.
Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kukiuka maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wengine wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.
Makamba amesamehewa, huku Kinana akionywa kwa karipio.
Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole alidai kuwa mwenendo wa Membe umekuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.
"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," alieleza Polepole.
Membe, Makamba na Kinana walipelekwa katika kamati ya maadili ya CCM mwezi Disemba mwaka jana, na taarifa ya chama hicho ilidai kuwa viongozi hao pamoja na makada wengine watatu ambao walisamehewa walikidhalilisha chama mbele ya Umma.
Makada ambao walitangazwa kusamehewa ni January Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja ambao wote walimuomba radhi mwenyekiti wa CCM na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.
Baadhi ya mazungumzo ya simu ya wanachama hao sita wa CCM yalivujishwa kwenye mitandao nchini Tanzania wakizungumzia masuala mbalimbali kukihusu chama na mwenyekiti wake.
Sehemu ya mazungumzo yaliyovuja ya Mzee Yusuf Makamba na Kinana ni pamoja na kuandaa taarifa ya malalamiko dhidi ya 'mawanaharakati' Cyprian Musiba ambaye wanamtuhumu kwa 'kuwadhalilisha' bila kuchukuliwa hatua yoyote na kuhoji analindwa na nani?