Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 5:01 pm

NEWS: MEMBE AAHIDI KWENDA KILA KONA YA NCHI KUTAFUTA USHINDI

Mgombea Urais wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ndugu Bernard Kamilius Membe amewaahidi wanaACT Wazalendo na watanzania kwa ujumla wake kwamba atakwenda kila kona ya nchi ya Tanzania kuhakikisha anakipa ushindi chama chake cha Sasa(ACT Wazalendo).

Membe ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya njee wa Tanzania ametoa kauli hiyo hii leo Agosti 7, 2020 baada ya kuchukua fomu ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika makao makuu ya Tume ya taifa ya uchaguzi nchini (NEC) Jedengwa jijini Dodoma.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu hizo, Bernard Membe amesema kuwa amejiandaa kufanya kampeni kabambe kila Kona ya nchi ili kuipatia ACT Wazalendo ushindi mnono na kuhakikisha ifikapo tarehe 28 Oktoba 2020, utawala wa Rais Magufuli unafikia tamati.

Julai 6, mwaka huu bwana Membe alirejesha kadi ya uanachama wa Chama cha CCM na Julai 15 akatangaza rasmi kujiunga na chama cha ACT Walendo.

Mwanadiplomasia huyo nguli wa zamani alirudisha kadi ya uanachama ingawa Chama cha Mapinduzi kilidai kuwa kilishamfukuza uanachama .

Membe alidai kuwa taratibu za kichama hazikufuatwa, na hivyo bado alikuwa mwanachama halali wa CCM.

Kwasasa Bwana Membe atakuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT Wazalendo baada ya kuombwa na viongozi na wanachama waandamizi wa chama hicho kuchukua fomu ya Urais.

Tuhuma dhidi ya Membe ndani ya CCM

Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kukiuka maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.

Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole alidai kuwa mwenendo wa Membe ulikuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.

"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," alieleza Polepole.

Membe alikuwa akituhumiwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho kuwa anajipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Membe alikuwa akihusishwa kwa muda mrefu na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi waliitafsiri kama usaliti.

Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais.