Home | Terms & Conditions | Help

November 23, 2024, 9:49 pm

NEWS: MCHUNGAJI MSIGWA AAHIDI KUFUMUA MFUMO WA ELIMU KAMA AKIWA RAIS

Dodoma. Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa ameainisha vipaumbele vitatu atakavyoanza navyo iwapo atapewa ridhaa ya kuiongza nchi, vipaumbele hivyo ni kuweka uchumi imara, kusimamia utawala bora na kuboresha elimu nchini.

Msigwa ametangaza rasmi nia yake hiyo ya kugombea Urais kupitia chama chake cha Chadema leo Juni 14, 2020 jijini Dodoma ambapo pia alisindikizwa na wabunge wenzake, Godbless Lema, Joseph Mbilinyi 'Sugu' Hawa Mwaifunga na John Heche.

Akizungumza na wandishi wa habari wakati wa kutangaza nia yake hiyo, Mch Msigwa amesema endapo atapata ridhaa ya kuwa Rais atahakikisha anafumua muundo mzima wa Elimu nchini na kuweka mwingine utakaokua na matokeo chanya kwa Taifa.

Amesema mfumo wa elimu uliopo hivi sasa unaegemea zaidi vyeti na wala hauwapi wasomi mwanga wa kuwa wataalamu wa kuvumbua zaidi badala yake wanakua tegemezi ilihali ni wasomi.

" Nikipata ridhaa ya kuwa Rais nitahakikisha nafanya maboresho makubwa kwenye elimu, ni lazima tuwe na Nchi ya wavumbuzi wanaotafuta suluhihisho kitaalamu, tuondokane na elimu ya vyeti ambayo kwa miaka 50 imeshindwa kuwakomboa watanzania.

Kama Taifa hatuwezi kufanikiwa kwa kuwa na watu wenye fikra ndogo, tofauti yetu na wenzetu walioendelea ni upanuzi wa fikra na ukubwa wa elimu yao, tunapaswa kuwekeza kwenye elimu kama kweli tunataka kufikia uchumi wa kati unaotokana na viwanda, " Amesema Mch Msigwa.

Akizungumzia ukuaji wa uchumi, Mch Msigwa amesema mfumo uliopo pia unahitaji mabadiliko makubwa kwani huu wa sasa umepitwa na wakati na hauwezi kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.

Amewaomba watanzania watakapoenda kuchagua Rais Oktoba 25 mwaka huu wachague Kiongozi mwenye maono ya kuwavusha kiuchumi na mwenye uwezo wa kuvutia wawekezaji na kutoa wigo mpana pia wa watanzania wenye kujiajiri.

" Suala la utawala bora nitalisamamia kwa kuhakikisha pia tunarudish mchakato wa katiba mpya ambao utawezesha kubadilisha sheria kandamizi ambazo zimekua hazina msaada kwa watanzania zaidi ya kuwakandamiza.

Kupitia mchakato wa katiba mpya naamini pia tutapata tume huru ya Uchaguzi ambayo itamaliza kiu ya watanzania lakini pia kuweka mgawanyo wa kimadaraka," Amesema Mch Msigwa.

Mch Msigwa anakua mwanachama wa tatu wa Chadema kutangaza nia ya kugombea Urais hadharani baada ya wanachama wawili Mayjose Majinge na Makamu Mwenyekiti wa Chadema hiko, Tundu Lissu kutangaza azma yao ya kugombea kupitia chama hiko kikuu cha upinzani.