Home | Terms & Conditions | Help

November 22, 2024, 8:28 pm

NEWS: MBUNGE WA TANZANIA AJIUZULU BILA KUPENDA

Dar es Salaam. Mbunge mteule wa jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki amejiuzulu nafasi hiyo kwa kile alichodai yeye mwenyewe kuwa ni kwasababu ya changamoto za kifamilia.

Kujiuzulu kwake kumepokelewa na chama chake cha mapinduzi CCM mara baada ya taarifa ya Chama kutolewa hii leo.

Faki alichaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 18 ambapo CCM ilishinda katika jimbo hilo pamoja na kata sita zilizoshiriki uchaguzi huo ambapo ilishinda bila kupingwa katika kata nne miongoni mwa hizo.

Taarifa za Ndani kutoka katika chama chake zinadai kuwa Mbunge huyo mteule amejiuzulu nafasi yake ili uchaguzi urudiwe kuiokoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ya Zanzibar mara baada ya chama ACT-Wazalendo kutishia kujitoa kutokana na tuhuma za dhulma na uonevu kwenye uchaguzi uliofanyika jimbo hilo la Pemba

Amejiuzulu kabla hajaapishwa na Spika wa Bunge zikiwa zimepita siku 14 tu tangu alipochaguliwa katika uchaguzi uliohusisha pia chama cha ACT-Wazalendo ambacho kilipoteza jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 2 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, Faki ameandika barua ya kujiuzulu ambapo ameeleza kufikia uamuzi huo kutokana na changamoto za kifamilia.

“Chama cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa barua ya kujiuzulu kwa mbunge wa mteule wa CCM jimbo la Konde, Sheha Mpemba Faki leo Agosti 2, 2021,” amesema Shaka katika taarifa yake.

Shaka amesema chama hakina uwezo wa kumzuia katika uamuzi wake huo hasa ikizingatiwa ni haki yake ya msingi kama ilivyo kwa haki ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ndani ya CCM.

“Chama cha Mapinduzi kinawaomba wanachama wote kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati tukisubiri taratibu nyingine,” inaeleza taarifa hiyo ya Shaka.